![]() |
| Sylvester Ambokile. |
Idara ya Uhamiaji imefanya mabadiliko makubwa katika safu za maofisa wake wa mikoa, wilaya na wafawidhi wa vituo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari na Uhusiano makao makuu ya Idara ya Uhamiaji, uteuzi huo uliofanywa na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile, baadhi ya maofisa wamepandishwa vyeo, wengine kuhamishiwa maeneo mengine kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa idara hiyo.
Ambokile ameteua, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Jacob Sambai aliyekuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Manyara kuwa Msaidizi wa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mtwara na nafasi yake kuchukuliwa na Naibu Kamishna Barikieli Shayo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Augustino Haule akiteuliwa kuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa Morogoro.
Katika mabadiliko hayo, Naibu Kamishna Hilgaty Shauri aliyekuwa Mdhibiti wa Pasipoti Makao Makuu anakuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kinondoni na nafasi yake kuchukuliwa na Naibu Kamishna Abuu Mvano ambaye kabla ya mabadiliko hayo alikuwa Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji cha Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Wengine ni Naibu Kamishna Fredrick Kiondo aliyekuwa Mfawidhi Kituo cha Holili ambaye sasa anakuwa Mfawadhi wa KIA wakati nafasi yake ikichukuliwa na Naibu Kamishna Estomih Urio ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Karatu. Naibu Kamishna Apolinary Msuya anakuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Karatu akitoka Ofisi ya Uhamiaji Tarakea mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Naibu Kamishna Evarist Mlay kutoka Tunduma anahamia Mkoa wa Dar es Salaam na nafasi yake kuchukuliwa na Naibu Kamishna Alphonce Kwikubya aliyekuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kinondoni akisaidiwa na Naibu Kamishna Lusarago Mreka kutoka makao makuu.
Naibu Kamishna Sipora Moshi aliyekuwa Mfawidhi Kituo cha Bandari ya Dar es Salaam sasa anakuwa Mkuu wa Kitengo cha Ubalozi Makao Makuu ya Uhamiaji na nafasi yake kuchukuliwa na Naibu Kamishna Harride Mwaipyana aliyekuwa Ofisi ya Uhamiaji Kabanga.
Wakati huo huo, mabadiliko hayo ambayo yanaanza mara moja ni sehemu ya kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji ndani ya Idara ya Uhamiaji katika kuhudumia wananchi, kuwezesha uingiaji na utokaji wa watu na udhibiti wa wageni nchini.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya, alisema Idara imeandaa mkakati wa maboresho ya kitaasisi, rasilimaliwatu pamoja na vitendea kazi ili kuhakikisha watumishi wanaondokana na utendaji wa mazoea.
ÒIdara ya Uhamiaji imeandaa Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao utazinduliwa hivi karibuni kwa nia ya kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa. Mkataba huo utawapa pia wadau wa huduma za uhamiaji, fursa ya kufahamu haki zao, wajibu walionao katika kupata haki hizo na mfumo wa kutoa mrejesho kuhusu huduma wanazopata,ÕÕ alifafanua.
Mabadiliko hayo yanakuja katika kipindi cha mwezi mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete amteue Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ambokile kuongoza Idara ya Uhamiaji, akichukua nafasi ya Magnus Ulungi ambaye amepangiwa majukumu mengine.
Lakini pia ni wakati ambao nchi imechafuliwa na vitendo vya usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia katika mipaka ya nchi hususan viwanja vya ndege.
Sambamba na hilo ni uingiaji holela wa wahamiaji haramu kupitia mipakani hususan Magharibi mwa nchi na baadhi ya miji huku juhudi ndogo zikifanywa na idara hiyo kudhibiti hali hiyo, hadi Rais Kikwete alipotangaza hivi karibuni operesheni maalumu ya kuwaondoa nchini.
Kabla ya uteuzi wake, Ambokile alikuwa Mwambata wa Uhamiaji katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.

No comments:
Post a Comment