![]() |
Balozi Job Lusinde. |
Alinusurika hivyo baada ya kuamuru kuweka lami kwenye njia ya vumbi kwenda nyumbani kwa Mwalimu, eneo la Msasani jijini Dar es Salaam.
Alisema hayo mjini Dodoma juzi wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 14 tangu kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Lusinde aliyewahi kuwa Waziri katika wizara mbalimbali, alisema wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, mwalimu alikopa fedha na kujenga nyumba katika eneo la Msasani, lakini barabara yote ya kwenda nyumbani kwake ilikuwa ya vumbi.
Alisema nyumbani kwa Mwalimu, walikuwa wakifika wageni mbalimbali wa kitaifa na kimataifa; kwa hiyo wizara yake ikaona lazima wafanye kila linalowezekana barabara hiyo iwekwe lami.
Lusinde alisema walivizia wakati hayupo; akiwa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa, wakaiweka lami barabara hiyo.
“Aliporudi, akaniita, akaniuliza Job, ni nani amefanya hivi? Kwa nini mnatumia fedha za wananchi kuweka lami kwenye nyumba yangu binafsi? Kisha Mwalimu akaondoka, nikasema hapa kazi imekwisha,” alisema Lusinde.
Aliongeza, “Nikamwambia wewe ni Rais wetu, kuna watu wengi wanakuja hapa, tukaamua tufanye papendeze, lakini akasema haitaki tena nyumba hiyo, anahama”.
Lusinde alisema Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi wa pekee, ambaye alikuwa akitaka kuishi maisha ya kawaida ya usawa, sawa na wananchi wengine; na alikuwa akiongoza kwa mfano.
Akielezea tukio la pili, Lusinde alisema lilimtokea wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ambapo Mwalimu Nyerere alikataa kusiwe na pikipiki kwenye msafara wake, jambo ambalo lilisababisha uongozi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama kutaka kumwajibisha, kwa kushindwa kumpa Nyerere ulinzi.
“Hapo ilibidi niseme ukweli, kuwa Rais ndiye alikataa msafara wake usiwe na pikipiki,” alisema.
No comments:
Post a Comment