![]() |
| Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam. |
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewahukumu kifungo cha kati ya mwaka na nusu na saba jela baadhi ya washitakiwa wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Waliohukumiwa jana ni watatu kati ya watano wakiwamo wana ndoa wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa Sh bilioni 1.1 zilizokuwa zikitunzwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Washitakiwa waliohukumiwa ni Bahati Mahenge ambaye atatumikia kifungo cha miaka saba, Manase Mwakale miaka mitano na mkewe Eddah Mwakale miezi 18.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na jopo la mahakimu watatu waliosikiliza kesi hiyo ambao ni Sam Rumanyika, Sekela Mosha na Lameck Mlacha.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya jopo, Mlacha alisema baada ya kupitia ushahidi ambao haukuwagusa washitakiwa Davies Kamungu na Godfrey Mosha walioachwa huru, uamuzi wa Mahakama dhidi ya washitakiwa waliotiwa hatiani unazingatia kifungo na washitakiwa kurejesha fedha walizoiba.
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, aliomba Mahakama kuangalia kuwa makosa waliyofanya washitakiwa hao ni makubwa na kuitia hasara Serikali, akaomba adhabu kali itolewe iwe fundisho kwa wengine.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Deogratius Lyimo aliomba Mahakama iangalie kuwa lilikuwa kosa la kwanza kwa wateja wake na kwamba kesi hiyo iliendeshwa kwa muda mrefu hivyouwepo uwezekano wa washitakiwa kupewa adhabu ndogo kwani bado wana nafasi ya kujifunza na kujirekebisha.
Akifafanua juu ya adhabu kwenye mashitaka saba yaliyowatia hatiani baada ya mawili kuondolewa, kwa kuwa upande wa mashitaka haukuyafanyia marekebisho kwa mujibu wa agizo la Mahakama, alisema kwa mashitaka ya kula njama, Mahenge na Manase watatumikia kifungo cha miaka mitano.
Kwa mashitaka ya kughushi Mahenge na Manase watatumikia kifungo cha miaka mitano jela, huku katika mashitaka ya kutoa hati ya kiapo iliyoghushiwa, ambayo yanamhusu Mahenge peke yake adhabu yake ni kifungo cha miaka saba jela.
Kwa upande wa mashitaka ya kusajili kampuni kwa nyaraka za kughushi, yaliyowahusu Mahenge na Manase watatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, ambapo pia Mahenge, Manase na Eddah, watatumikia kifungo cha miezi 18 jela.
Kuhusu mashitaka ya kughushi hati ya makubaliano ya kuhamisha deni kutoka kampuni ya Marubeni Co-operation ya Japan kwenda kampuni yao ya Changanyikeni Residential Complex, Mahenge na Manase wanakwenda jela miezi 18 na kwa mashitaka ya kutoa nyaraka zisizo sahihi BoT yanayomhusu Mahenge peke yake anakwenda jela miaka mitano.
Kabla ya uamuzi huo, akichambua ushahidi wa kila mashitaka yaliyokuwa tisa wakikabiliwa nayo washitakiwa wote watano, Mlacha alisema katika mashitaka ya kwanza Mahenge na Manase kulingana na ushahidi walionesha kusaidiana kula njama.
"Kwa mujibu wa ushahidi mshitakiwa wa kwanza na wa pili ilielezwa walisaidiana kupata fedha hizo, ikionesha palikuwa na mpango wa kuzipata, lakini kwa washitakiwa wengine hakuna kinachoonesha kuwaunganisha katika mashitaka hayo," alisema Mlacha.
Mlacha aliongeza kuwa ilithibitika pia kwamba washitakiwa hao walijua jina walilotumia la Samson Mapunda kuwa ni la kufikirika, lakini wakalitumia ambapo kwa Mahenge ushahidi ulithibitisha kuwa alilitumia.
Alisema upo ushahidi ulioonesha washitakiwa wa tatu na wa nne, kuwa walipokea hundi, hivyo upande wa mashitaka uliiomba Mahakama kuwaona wana hatia, lakini walishindwa kupokea maombi hayo kutokana na hundi aliyolipwa mshitakiwa wa tatu malipo ambayo yalifanyika kabla ya fedha kuingia katika akaunti hiyo ya BoT.
Aidha, alisema mshitakiwa wa nne, kwa mujibu wa shahidi wa nane alipewa hundi ya Sh milioni 200.
Mahakama hiyo ilisema inaondoa mashitaka ya nane na tisa si kwa sababu washitakiwa hawakutenda, lakini ni kwa kuwa yalikuwa na upungufu, hivyo kuhitaji kurekebishwa na upande wa mashitaka, lakini mawakili wake hawakufanya hivyo.
Akiwa nje ya Mahakama, Wakili Lyimo alisema hajaridhika na hukumu kwa wateja wake na kufafanua: "Kwa sababu ukiangalia ni kama vile kuna baadhi ya maeneo yalikuwa yakipindishwa, hivyo tukishapata nakala ya hukumu na kuipitia tutakata rufaa".
Baada ya hukumu hiyo baadhi ya ndugu walionekana kujawa na majonzi na huzuni huku wengine wakilia, ambapo Manase na Bahati walikumbatiana na ndugu na jamaa zao, lakini Eddah aliondoka huku akionesha alama ya dole gumba.

No comments:
Post a Comment