WACHUNGAJI WAHAMIAJI HARAMU WAKAMATWA KANISANI DAR...

Msako wa wahamiaji haramu kupitia Operesheni Kimbunga inayoendelea nchini, umejikita kanisani kutokana na wahamiaji haramu sita wa Nigeria, kubainika wakijishughulisha na kazi za kichungaji.

Akizungumza jana kwa niaba ya Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Sylvanus Mwakasekele, alisema wahamiaji hao walikuwa katika Kanisa la Praise la Tabata.
Kwa mujibu wa Mwakasekele, Uhamiaji walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwapo kwa wahamiaji hao kwenye Kanisa hilo.
Baada ya taarifa hiyo, alisema maofisa Uhamiaji walifika kanisani hapo juzi saa tano asubuhi na watu hao walipogundua, waliruka madirishani kukwepa mkono wa sheria na kukimbia wakitumia gari dogo aina ya Toyota Vitz.
"Walipokimbia walikuwa sita, vijana waliokwenda kufanya kazi hiyo waliwafuatilia na walipoona wako hatarini kukamatwa walitelekeza gari na kukimbia kwa miguu na kukamatwa wanne huku wawili wakitoroka,” alisema Mwakasekele na kuongeza kuwa wako katika harakati za kusaka waliokimbia. 
Aliwataja waliokamatwa na jinsi walivyoingia nchini, ni Moses Opara mwenye pasipoti namba A04809965, ambaye alikuwa kiongozi wa Kanisa hilo na ameishi nchini kwa miaka mitatu.
James Ateli mwenye pasipoti namba A04665804, aliyeingia nchini kama mfanyabiashara na kuishi kwa mwaka mmoja.
Pia Keneth Onyebuchi aliyeingia nchini kama mfanyabiashara tangu Januari na kudai kupoteza pasipoti yake alipoingia nchini na mwingine ni Augustine Ndubilisi aliyeishi nchini mwaka mmoja.
"Huyu Augustine anadai anaishi na familia ya mchumba wake Mtanzania aliyetajwa kwa jina la Caro Mdegela, msichana huyu tunamshikilia kwa kuhifadhi wahamiaji haramu,” alisema.
Alisema baada ya kukamilika kwa mahojiano na watu hao, watafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuishi nchini bila kibali muda wowote kuanzia leo.
Mwishoni mwa wiki, Uhamiaji ilikamata Mchungaji wa Kanisa la Kimataifa la Life Chande Chapel lililoko Sinza E na watu wengine sita.
Wakati huo huo, mamia ya raia wa Malawi jana walifurika kwenye ofisi za Uhamiaji Dar es Salaam kujiorodhesha.
Mwandishi alifika katika ofisi hizo na kushuhudia umati wa vijana wa kike na kiume wakiwa na fomu walizojaza kuelezea uraia wao na anuani ya mahali wanakoishi nchini.
Watu hao ambao walionekana kutulia huku wakizungumza kwa lugha yao, walikuwa kwenye misururu mirefu kusubiri zamu za kuingia kuhudumiwa.
"Tangu asubuhi tumeanza kuwaorodhesha na mpaka sasa (saa nne kasoro asubuhi) mamia ya Wamalawi wameandikishwa na kurejea kwao,” alisema Mwakasekele.
Alisema katika uandikishaji huo, walitoa kipaumbele kwa wajawazito na wenye watoto, ili kuwapa nafasi ya kurejea kwao mapema.
"Kumekuwa na mwitiko mkubwa na hapa tumelazimika kuacha shughuli zingine za kila siku ili kuwahudumia wao, lengo ni tumalize kazi hii mapema. Lakini bado hatujafikia uamuzi wa lini uwe mwisho wa kuwaorodhesha,” alisema.
Katika kukamilisha kazi hiyo, Uhamiaji imetenga vyumba vitano vyenye maofisa watatu kila kimoja, ambao kazi yao ni kuorodhesha Wamalawi hao ambao walikuwa wakiingia kwa makundi. 

No comments: