SIXTUS MAPUNDA ATEULIWA KATIBU MKUU MPYA WA UVCCM...

Mkutano wa UVCCM.
Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), limemwidhinisha kwa kauli moja aliyekuwa Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda, kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa.

Kikao hicho maalumu cha Baraza Kuu kilichofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi, pia kimeidhimisha Naibu katibu wakuu, Mfaume Ally Kizigo (Tanzania Bara) na Shaka Hamdu Shaka (Zanzibar) waendelee na nafasi zao.
Akifungua kikao hicho, Balozi Iddi alitaka UVCCM iongeze mshikamano miongoni mwao na kukwepa makundi ili jumuiya hiyo iwe chachu ya uimara wa CCM.
Aliwataka viongozi na wanachama wa jumuiya hiyo kuwa makini na baadhi ya viongozi ambao kazi yao ni kutengeneza makundi, ili kuwatawanya kifikra, huku wakitumia nguvu ya fedha.
"Kama mnataka kuwa jumuiya yenye nguvu zaidi lazima mkwepe mianya na sababu zinazoweza kuwaingiza katika mgawanyiko unaosababishwa na makundi. Makundi hayajengi, yanaumiza chama.
"Tazama juzi juzi, ilitulazimu kujadili suala la Bukoba, tukaumiza vichwa kuhakikisha linakwisha, sababu haikuwa nyingine ni makundi tu, jamani sote ni wamoja ndani ya chama," alisisitiza Balozi Iddi.
Awali viongozi waliopata fursa ya kuzungumza kwenye mkutano huo, waliitaka UVCCM kuendelea kuwa imara kwa kufanya kazi zake kwa kuzingatia Katiba na   kanuni za chama.
"Jambo muhimu ni kuzingatia sheria na utaratibu wa jumuiya na chama. Mkizingatia hili mkaacha unafiki jumuiya hii inakuwa ya kupigiwa mfano.
“Vijembe hivi mnavyopigana wenyewe kwa wenyewe vielekezeni kwa wapinzani wetu kina Chadema," alisema Mwenyekiti wa Baraza la Udhamini la UVCCM na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.
Kwa upande wake Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliitaka UVCCM kuendelea kuwa jumuiya yenye nguvu na imara kwa kuwa ndiyo msingi wa uongozi bora.
"Jitahidini kuijenga UVCCM iendelee kuwa na sifa ile ile ya kuwa chanzo cha kutengeneza viongozi walio bora wa CCM. Kama mimi kuna kazi nzuri ninayofanya kwenye uongozi wangu wa sasa, basi ni matunda ya UVCCM," alisema Nape.
 Akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM aliyemaliza muda wake, Martine Shigela, alisema hana shaka yoyote na utendaji wa Mapunda kwa kuwa ni zao la UVCCM.
Alimtaka Mapunda kuwa karibu na viongozi na wafanyakazi wa UVCCM katika maeneo yote, huku akiwasihi viongozi na wafanyakazi kumpa ushirikiano ili atekeleze majukumu yake kwa ufanisi.

No comments: