RAIS MSTAAFU BUSH WA MAREKANI 'AMUUA MZEE MANDELA'...

KUSHOTO: Jim McGrath. KULIA: Gari la wagonjwa lililombeba Mzee Mandela kwenda nyumbani kwake mjini Johannesburg jana.
Rais wa 41 wa Marekani, George H.W. Bush alitangaza jana asubuhi kifo cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kabla ya wakati.

Mkanganyiko huo ulitokea pale msemaji wa Rais Bush, Jim McGrath aliposoma visivyo dondoo za habari za Washington Post.
"Taarifa ya Rais wa 41 iliyotumwa asubuhi hii ilikuwa matokeo ya kusomwa visivyo kichwa cha habari kwenye dondoo za habari za Washington Post. Nimefanya kosa la kipumbavu. Nawaomba radhi wote," Jim alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter jana asubuhi.
Taarifa halisi inasomeka: "Barbara na mimi tunaomboleza kifo cha mmoja wa waamini wakubwa wa uhuru tuliobahatika kuwafahamu. Kama Rais, nilitazama kwa maajabu wakati Nelson Mandela alivyokuwa na uwezo wa kuwasamehe waliomfunga jela kufuatia miaka 26 ya kifungo - akionesha mfano wenye nguvu wa ukombozi na hisani kwetu sote. Alikuwa mtu wa hamasa ya hali ya juu, ambaye alibadilisha historia ya nchi yake. Barbara na mimi tuna heshima kubwa kwa Rais Mandela, na kutuma rambirambi zetu kwa familia yake na watu wake."
Ofisi ya Rais Afrika Kusini ilirekebisha taarifa hiyo, ikisema Mandela bado yuko hai.
"Ni dhahiri sio sahihi. Tunaona kama ni kosa kwa upande wake" na haielekei "kufanya jambo kubwa", alisema msemaji wa Ikulu Mac Maharaj.
Nelson Mandela aliruhusiwa kutoka hospitalini jana baada ya mwanzoni kuwa amelazwa Juni kwa maambukizi kwenye mapafu. Bado hali yake ni mbaya.
Mzee Mandela alipakiwa kwenye gari la wagonjwa kuelekea kwake mjini Johannesburg ambayo imeandaliwa kutoa huduma za uangalizi maalumu.
Katika taarifa yake, serikali ilisema: "Hali ya Madiba bado ni mbaya na wakati fulani ni tete."
Rais wa zamani Bush pia anashughulikia matatizo yake binafsi ya kiafya.
Alishindwa kuhudhuria kumbukumbu ya Martin Luther King Jr. Jumatano iliyopita sababu umri wake mkubwa umesababisha sasa kutegemea kiti cha magurudumu.

No comments: