RAIS KIKWETE KUSAINI MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA....

Rais Jakaya Kikwete.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, amesema Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, utasainiwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa uliwasilishwa na kupitishwa bungeni kwa kufuata taratibu na kanuni zinazotakiwa.

Aidha, Chikawe ametaka wanaohamasisha wananchi kupinga Muswada huo na kutoa kauli za vitisho kuwa Rais akiusaini vurugu itatokea na damu kumwagika, waweke wazi namna vurugu na damu hiyo itakavyomwagika.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua jengo la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana, Waziri alisema Muswada huo uliwasilishwa bungeni na kupitishwa kwa kufuata taratibu zote, hivyo una sifa za kusainiwa na Rais.
“Nimesikia kuna watu wanahamasisha wananchi wapinge na kumtaka Rais Kikwete asiusaini, hayo ni mengine ila mimi nitashangaa iwapo Rais hatausaini, kwa kuwa umefuata taratibu zote na asipousaini italeta mgogoro na Bunge,” alisema Chikawe.
Alisema tangu Mei 27, Wizara yake ilipokea maoni juu ya Muswada huo kutoka Zanzibar ambako Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilichangia na maoni yao kutumika kuboresha Muswada huo kabla haujawasilishwa bungeni.
Alisema taratibu zote zilifuatwa tangu kuandaliwa kwa marekebisho, ushirikishwaji wananchi kutoa maoni na uwasilishwaji wake bungeni ambako taratibu zote zilifuatwa kwa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Upinzani kuwasilisha maoni yao juu ya Muswada huo.
“Kilichokuwa kinafuata pale ni majadiliano ya namna ya kuboresha Muswada huu, kwa kuwa si kila kitu tunachowasilisha bungeni kama Serikali ni lazima kipite hivyo kilivyowasilishwa, vinginevyo kungekuwa hakuna maana ya majadiliano, lakini katika hili bahati mbaya wenzetu wapinzani walitoka nje badala ya kuchangia,” alisema.
Chikawe alisema kwa upande wa Kamati ya Bunge ya Katiba nayo iliratibu maoni ya wadau ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara hiyo na kufanyiwa kazi.
“Kamati hizi huwa na utaratibu wao ama ziite wadau ili kupata maoni yao au kuwafuata waliko, Kamati hii haikwenda Zanzibar, hilo halinihusu kwa kuwa ule ni mhimili unaojitegemea siwezi kuuingilia, kama hawakwenda hilo halizuii kitu, kwa kuwa mwisho wa siku Muswada ulipitishwa na Bunge,” alisisitiza.
Alisema pamoja na ukweli huo wapo baadhi ya watu na vyama vya siasa wanaosambaza na kuhamasisha wananchi kuwa endapo Muswada huo utapitishwa damu itamwagika. “Sasa nawaambia, Muswada utasainiwa kwa kuwa una sifa zote, na kuhusu damu kumwagika waseme wao ndio wataimwaga, maana damu haiwezi kumwagika yenyewe.”
Alisema kipengele kinachopigiwa kelele kwenye Muswada huo ni cha ibara ya 26 ambapo wengi wameonesha wasiwasi kuwa Katiba inaweza kupitishwa na wabunge wa Bunge la Katiba wasiotimia theluthi mbili, jambo ambalo kupitia marekebisho hayo mapya, kuna mapendekezo ya namna ya kuondokana na hatari hiyo.
Aliongeza kuwa Muswada huo unaonesha wazi kuwa ili Katiba ipite, lazima ipitishwe na kukubaliwa na theluthi mbili ya wabunge wa Bunge hilo, iwapo kutatokea kutokubaliana kuhusu baadhi ya vifungu, wabunge hao watapigia tena kura vifungu husika na ikishindikana vitapigiwa kura na wananchi.
“Sasa kama katika kipengele hiki kuna kosa, basi watwambie njia nzuri ya kulitatua hili lakini pia kwa bahati mbaya hawakutumia nafasi waliyokuwa nayo, matokeo yake wakakimbilia na kupeleka maoni yao Jangwani. Sasa huko Jangwani kutasaidia nini? Muswada umeshapita sasa,” alisema Chikawe.
Hivi karibuni katika Mkutano wa Bunge uliopita majadiliano ya Muswada huo yalizua mtafaruku baina ya wabunge wa upinzani na Serikali wakitaka majadiliano hayo yasitishwe kwa kuwa marekebisho hayakushirikisha wananchi wa Zanzibar.
Pamoja na mtafaruku huo uliosababisha wabunge kutoka bungeni, mjadala wa Muswada huo uliendelea na kupitishwa jambo lililosababisha, vyama vya siasa vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kuunda ushirikiano dhidi ya Muswada huo.
Juzi wenyeviti wa vyama hivyo ambao ni Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema) na James Mbatia na baadhi ya wanaharakati, walitoa tamko la kumwomba Rais Kikwete asiusaini kwa madai kuwa una upungufu.
Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imepiga marufuku maandamano ya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kutokana na kuwapo uwezekano wa uvunjifu wa amani.
Badala yake imeruhusu mkutano ambao ulipangwa kufanyika katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema walipokea barua isiyo na namba ya kumbukumbu   kutoka kwa makatibu wakuu wa vyama hivyo ikitoa taarifa ya kusudio la kufanya maandamano na mkutano wa hadhara kesho.
Lengo la mkutano huo ni kuhamasisha wananchi kushiriki mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya na yalikuwa yafanyike kuanzia saa 6 mchana eneo la Vetenari  kupitia barabara ya Nelson Mandela , Buguruni Sheli, Uhuru, Karume Shule ya Msingi, Uhuru Mchanganyiko, Fire hadi Jangwani.
Kova alisema barua hiyo ilieleza kuwa mkutano huo utaongozwa na viongozi wa kitaifa wa vyama hivyo.
“Tulipitia barua na kubaini kuwa, kwa vile kusudio la mkutano ni kuhamasisha wananchi kushiriki mchakato wa Katiba mpya, hilo limeonekana si tatizo kiusalama kwa kuwa askari watalinda mkutano huo.
Kuhusu maandamano alisema Polisi haioni sababu za msingi za kuandamana   kwani upo uwezekano wa kutokea kwa uvunjifu wa amani.
“Sehemu zote yatakapopita maandamano hayo ni maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu ambao watakuwa katika shughuli za kiuchumi, kiusafiri na mahitaji ya dharura ya kibinadamu kama vile ugonjwa na dharura nyingine ambazo haziepukiki.
“Aidha zipo taarifa za kiintelijensia kuwa vyama hivyo vinaendeleza uhamasishaji   kwa waendesha pikipiki, maguta na waenda kwa miguu kujikusanya katika maeneo hayo ili kuelekea Jangwani,” alisema Kamanda Kova.
Alisema wakiruhusu maandamano hayo yatasababisha usumbufu kwa watu wengine na uvunjifu wa amani na malalamiko kwa jamii.

No comments: