RAIS KABILA NA WAASI WA M23 WATAKIWA KUZUNGUMZIA AMANI DRC...

Rais Joseph Kabila.
Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu umewapa siku 17 waasi wa M23 na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumaliza mgongano baina yao kwa njia ya amani.

Katika siku hizo, tatu zinapaswa kutumika kwa maandalizi huku 14 kwa kuhakikisha wanamaliza mgongano huo kwa mazungumzo jijini Kampala, chini ya msuluhishi wa mgogoro huo wa tangu mwaka 2008 Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.  
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alipokuwa akielezea maazimio ya kikao cha wakuu wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kilichomalizika juzi Uganda.
Alisema lazima katika siku hizo, pande hizo zihakikishe zinamaliza mgogoro wao   kwa njia ya amani kabla hatua zingine hazijafuata.
Pia alisema nchi hiyo kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN) wameazimia kuhakikisha vikundi vyote vya uasi DRC vinaacha mapigano kabla ya hatua nyingine.
“Wakati nchi hizo zikishughulikia  waasi wengine wakiwamo wanaojiita Cobra, ADF, FDLR na wengine, Rais Museveni aliagizwa katika siku hizo kuhakikisha anamaliza mgogoro wa waasi wa M23 kwa amani,” alisema Membe.
Alisema pia wajumbe wa mkutano huo uliokuwa na lengo la kutafuta suluhu ya vita DRC, walilaani mashambulizi ya kundi la M23 kujeruhi wananchi na kutoa pole kwa Umoja wa Mataifa (UN) na Tanzania kwa kumpoteza Meja Khatibu Mshindo na wengine kujeruhiwa ambao wanaendelea vema.
“Hivyo kwa pamoja wamekubaliana kufanyika kwa uchunguzi kubaini mabomu yaliyopigwa katika mji wa Goma yalitoka nchi gani na kutumika kujeruhi wananchi wa mji huo,” alisema Membe.
Membe alisema katika mkutano huo uliochukua saa moja baina ya Rais Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda, ulimalizika kwa maelewano na kuwa chanzo cha mikutano mingine ili kufikia mwafaka na kurudi katika uhusiano wa awali.
Alisema mkutano huo ulikwenda vizuri na ukiwa wa kuelimishana na kueleweshana kile ambacho kila mmoja alikisikia na kuendelea na mikutano, ili kuepusha migogoro iliyotaka kuibuka na kusababisha kukosekana kwa amani.
Membe alisema Rais Kikwete alifanya mazungumzo na Rais Museveni kuhusu suala la kufukuza wakimbizi na kumweleza kuwa  si la kweli hakuna mkimbizi aliyefukuzwa, bali wahamiaji haramu ambao walipewa wiki mbili kujiandikisha au kuondoka wenyewe.
Pia alimweleza kuwa si kweli kuwa suala hilo lililenga kufukuza raia wa Rwanda kwani kati ya wahamiaji waliorudi kwao, Warundi ni 21,000 na Wanyarwanda ni 6,000 pamoja na mataifa mengine.
“Katika hili hatujavunja sheria, kwani bado tuna wakimbizi 220,000 ambao wako chini yetu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR)  ambao hawajasema lolote kama tungekuwa tumefukuza wakimbizi," alisisitiza.
Katika suala hilo, Rais aliwaagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kulishughulikia bila kusababisha usumbufu na kero kwa Taifa.
“Kama kuna mtu aliyefukuzwa na kuona haikuwa halali, tunamwomba arudi hata leo na kuonana na maofisa Uhamiaji na kujiandikisha, kwani wapo walioondoka kwa kufuata mkumbo,” alisema.
Membe aliwataka Watanzania kutohangaika kwa baadhi ya nchi kufanya mikutano bila kushirikisha Tanzania kwani hilo linaruhusiwa, lakini ni lazima kutoa taarifa kwa jumuiya kubwa  na nchi zingine kupata maelezo.
Alisema  anachoamini kuwa kilichotokea kwa Uganda, Kenya na Rwanda kukutana bila wanachama wengine, kilikuwa kwa nia njema na kama ni mbaya anaamini yatarekebishwa, kwani hakuna namna ya kuitenga Tanzania katika nchi za Afrika Mashariki.
Membe alisema kati ya nchi 33 zilizosaini mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) za Afrika wanatarajia kukutana Januari ili kufikia mwafaka iwapo waendelee na mkataba huo au wajitoe.
Hatua hiyo inafikia baada ya kuonekana mahakama hiyo kama ipo kwa ajili ya viongozi wa Afrika na si mabara mengine ambao wanaweza kutenda kosa moja, lakini hatua zikachukuliwa kwa Afrika pekee.
Kuhusu mgogoro wa Tanzania na Malawi, Membe alisema kwa sasa kesi iko chini ya marais watatu wastaafu wa Afrika na jopo la wanasheria saba  wakubwa ulimwenguni.
Alisema kwa sasa wanasubiri kuitwa na jopo hilo, yeye na Mwanasheria wa Serikali atakayekuwa na jopo lake na wako tayari kutoa utetezi wao na kusubiri uamuzi.
Membe alisema Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina na wenzake watatu wamejitoa katika uchaguzi wa nchi hiyo unaotarajia kufanyika mwezi ujao ukiwa na wagombea 33 huku ukitarajiwa kufanyika kwa awamu mbili.

No comments: