MZEE MANDELA ATOKA HOSPITALI, MADAKTARI WAHAMIA NYUMBANI KWAKE...

Gari la wagonjwa linaloaminika kumbeba Mzee Mandela (picha ndogo) kuelekea nyumbani kwake.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ameruhusiwa kutoka hospitali na sasa yupo katika makazi yake jijini Johannesburg, akiendelea kupewa uangalizi wa karibu wa afya yake, Ikulu ya Afrika Kusini imesema katika tovuti yake.

Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya maofisa wa Serikali awali kukanusha taarifa zilizotangazwa na vyombo vya habari kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 95, alikuwa ameruhusiwa kutoka hospitalini.
Hata hivyo taarifa hiyo ilisema hali ya kiongozi huyo  bado ni mahututi ingawa imetulia.
Rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini, amekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Medi-Clinic ya Pretoria tangu Juni mwaka huu.
"Jopo la madaktari wanaomtibu wamesema wataendelea kumpatia uangalizi wa juu kabisa wa afya yake akiwa nyumbani kwake Houghton kama vile ilivyokuwa alipokuwa hospitali,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, familia imeafiki mpango huo wa kumpatia Mandela matibabu akiwa nyumbani kwa vile ataendelea kutibiwa na madaktari wenye utaalamu wa juu kama wale waliopo hospitali.
Katika hatua nyingine taarifa hiyo ya Ikulu ya Afrika Kusini ilisema; “ Kama italazimika, atarejeshwa tena hospitali.”
Hatua ya Mandela kuruhusiwa kutoka hospitalini, ni faraja kubwa kwa familia na dunia ambayo ilikuwa katika hali ya taharuki iliyosababishwa na kuzorota kwa afya yake.
Mtoto wa mwisho wa Mandela, Zindzi aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba kuna wakati hata familia ilikuwa na hofu kuhusu hali ya baba yao.
"Kuna wakati wote tulikuwa na hofu kubwa na tulijiandaa kwa chochote kibaya,” alikaririwa akisema. 
Naye mjukuu wa Mandela, Mandla aligeuka gumzo wakati wa ugomvi wa familia ya kiongozi huyo wa mahali pa maziko yake, uliosababisha makaburi ya watoto watatu wa kiongozi huyo, kufukuliwa na kuhamishwa.
Mahakama ilimuamuru Mandla, Chifu wa Mvezo alikozaliwa Mandela, aruhusu makaburi hayo yafukuliwe na mabaki ya miili hiyo ikazikwe Qunu, alikokulia Mandela.
Mzozo huo ulidaiwa kusababishwa na wosia wa Mandela kutaka azikwe karibu na walipozikwa watoto wake, wakati Mandla alihamisha makaburi hayo miaka miwili iliyopita kutoka Qunu kwenda Mvezo.

No comments: