Sunday, September 29, 2013

MAWAZIRI WANNE KENYA WALIPUUZIA ONYO LA MAGAIDI WA AL SHABAAB...

Moshi ukifuka kwenye jengo la Westgate Shopping Mall, mjini Nairobi.
Mawaziri wanne na Mkuu wa Majeshi wa serikali ya Kenya walionywa kuwa kundi la kigaidi la al-Shabaab linapanga kufanya mashambulizi jijini Nairobi ambapo watavamia jengo na kushikilia  watu mateka.

Tahadhari hizo zilianza kutolewa Januari mwaka huu na ziliongezeka mapema mwezi huu wakati mawaziri ambao ni wajumbe wa Baraza la Usalama wa Taifa waliambiwa kuwepo kwa mipango ya kusababisha ghasia mjini Nairobi na Mombasa, Kenya siku ya Septemba 13 na 20 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti ya ugaidi ambayo gazeti la Saturday Nation imeiona, Waziri wa Fedha Julius Rotich; Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph ole Lenku ; Waziri wa Mambo ya Nje, Amina Mohammed; Waziri wa Ulinzi, Raychelle Omamo na Mkuu wa Majeshi  Kenya, Jenerali Julius Karangi, wametahadharishwa kuhusiana na kuwepo kwa mipango ya mashambulizi nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, magaidi walipanga kuvamia kwa mtindo wa Mumbai kwa kuvamia jengo wakiwa na bunduki na mabomu na kwamba walipanga kushikilia watu mateka.
“Walipewa taarifa za awali wakifahamishwa kuwepo kwa ongezeko la tishio la ugaidi na mipango ya mashambulizi mfululizo Nairobi na Mombasa Septemba 13 na 20, 2013,” ilisema ripoti hiyo.
Taarifa hizo pia za awali ilipewa Kamati ya Ushauri ya Usalama wa Taifa katikati ya Septemba, wakati ripoti za kiintelijensia kuonesha shughuli za al-Shabaab nchini Kenya na walikuwa wakipanga kufanya mashambulizi.
Kamati hiyo ni chombo cha juu cha ulinzi Kenya. Kamati hiyo inamhusisha Rais, Naibu Rais, Mawaziri wa Ulinzi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu, Mkuu wa Majeshi, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na Inspekta Jenerali wa Polisi. 
Haijawekwa wazi iwapo Rais aliwahi kupewa taarifa hizo za awali za tahadhari. Tukio la mashambulizi katika kituo cha kibiashara cha Westgate lililotokea Jumamosi iliyopita ya Septemba 21 na kuua watu 67 na kujeruhi 175, ikiwa ni siku moja baada ya siku iliyokuwa imekadiriwa kufanyika mashambulizi hayo.
Mashambulizi yaliyofanyika Westgate, kituo cha kibiashara kinachomilikiwa na raia wa Israel, kinatokana na tahadhari zilizowahi kutolewa na Israel kwa serikali ya Kenya.
Israel ilisema magaidi wanapanga kushambulia maeneo yanayomilikiwa na raia wake wakati wa Sikukuu ya Wayahudi kati ya Septemba 4 na  28.
“Ubalozi wa  Israel mjini Nairobi uliieleza Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya kuwa Iran na Hezbollah kutoka Lebanon wamekuwa wakikusanya habari za kiintelijensia za pamoja na maeneo ya  shabaha ya Waisraeli na Wayahudi duniani ikiwemo Kenya,” ilionya ripoti iliyotolewa Septemba 13, 2013.
Maeneo mengine ya shabaha yaliyotajwa ni kwenye mitambo ya Marekani na Uingereza na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ambayo haikuwekwa wazi.
Ripoti hiyo ilimtaja mtu aliyeitwa kwa jina la Ahmed Imam Ali kama mtu anayepanga mashambulizi katika mitambo hiyo.
Mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo hawakupatikana kutoa maoni yao na ujumbe mfupi uliotumwa katika simu zao haukuleta majibu yoyote.
Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya kiintelijensia, Westgate na  Holy Family Basilica mjini Nairobi ni maeneo yaliyopangwa kushambuliwa mapema mwaka huu.
Ripoti hiyo inamtaja Shehe Abdiwelli Mohammed na Shehe Hussein Hassan kuwa vinara wa mpango huo.
“Wanaaminika kuwa tayari walishafanya utafiti wa maeneo ambayo wameyachagua kuwa shabaha yao ya kushambuliwa,” ilisema ripoti hiyo.
Inaelezwa kuwa shambulizi  la Westgate liliamriwa na Kiongozi wa  al-Shabaab, Abdi Godane na kwamba baadhi ya magaidi walioshiriki wametokea eneo la  Bullo Marer karibu na  Barawa, Somalia.
Godane ni Kiongozi mpya wa  al-Shabaab baada ya kumuua Omar Shafik Hammami na kumfukuza Sheikh Aweys, ambaye baadaye alijisalimisha kwa serikali ya Somali.
Katika hatua nyingine, Maofisa Wakuu wa Ujasusi wametakiwa kufika mbele ya Kamati ya Ulinzi ya Bunge ili kuhojiwa kuhusu mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Kituo cha Biashara cha Westgate mjini Nairobi.
Taarifa kwenye vyombo vya habari nchini humo zinaonesha kuwa hali ya kulaumiana imeanza kuibuka huku mashirika ya usalama yakinyosheana kidole.
Wataalamu wa uchunguzi wa mauaji wangali wanafanya uchunguzi wao wakitafuta miili na dalili za kilichosababisha shambulizi hilo.
Kamati ya bunge inataka maofisa wanaohusika na masuala ya usalama wawajibishwe.
Kundi la kigaidi la nchini Somalia, al-Shabaab limedai kufanya mashambulizi hayo yaliyodumu siku nne kama hatua ya kulipiza kisasi kwa Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.Hatua ya kuwataka maofisa hao wa usalama kufika mbele ya tume ya bunge siku ya Jumatatu, inakuja kutokana na wasiwasi miongoni mwa Wakenya kuhusu kiwango cha maofisa hao kujiandaa kwa tukio lolote la kigaidi sawa na lililotokea Westgate.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari mmoja wa maofisa waliotakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ni Mkuu wa Shirika la Ujasusi Michael Gichangi, anayesema alitoa taarifa za ujasusi kuhusu shambulizi hilo kwa polisi.
Hata hivyo, Ofisa mmoja mkuu katika Idara ya Polisi alikana kuwa taarifa hiyo ilitolewa kwa polisi.
Ingawa tukio la mashambulizi ya kigaidi yamefanyika Nairobi ikiwa ni mbali na Uingereza ambayo ndio nchi yenye jamii kubwa ya Wasomali,   raia hao wana hofu tukio hilo kuwaathiri.
Raia 100,000 wa Somali wanaoishi Uingereza walishikwa na kihoro baada ya kundi la kigaidi la wapiganaji wa Somali la Al Shabaab kudai kuhusika na shambulizi hilo na kwamba ni fedheha tena kwao kwa nchi yao kupamba vichwa vya habari kwa sababu mbaya.
Katika kitongoji cha Harlesden kilichopo kaskazini magharibi mwa mji wa London ambacho wanaishi Wasomali wengi, wanaume wanasikika wakizungumza kwa uchungu kushutumu wapiganaji hao wa al-Shabaab ambao wanahusishwa na kundi la Al-Qaeda wakiwa katika migahawa, sokoni na maduka ya huduma za intaneti.

No comments: