Sehemu ya bandari ya Dar es Salaam. |
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amebaini kuwepo kwa wizi mkubwa wa mafuta aina ya petroli katika bandari ya Dar es Salaam unaofanywa na mzungu anayetajwa kuiba kiasi cha lita 20,000 kila siku baada ya kutoboa boya kubwa la kupakulia mafuta (SBM).
Ingawa haukutajwa uraia wa mzungu huyo, imeelezwa baada ya kuiba kiasi hicho kikubwa cha petroli akiwatumia walinzi wa kitanzania, hujaza kwenye maputo.
Hayo yalibainika jana wakati Waziri Mwakyembe alipofanya ziara na kuzungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Wakala wa Ndege za Serikali.
Akiwa bandarini, Dk Mwakyembe aliahidi kupambana na mzungu huyo anayetumia walinzi wa kitanzania wa kampuni inayolinda boya hilo ambayo hakuwa tayari kuitaja kwa jina kwa kuhujumu nchi na kusema ataondoa ‘uzungu wake’ unaompa kiburi cha kufanya wizi. Haikuelezwa amefanya wizi huyo kwa muda gani.
Alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini wanafanya kazi hiyo kutafuta aliyewatuma watu hao akiwemo mzungu huyo ili kuweza kumchukulia hatua za kisheria.
“Nitapambana na huyo mzungu kwa nguvu zangu zote na kuondoa uzungu wake ili kumfikisha katika vyombo vya sheria,” alisema huku akionesha picha ya boya hilo lilivyotobolewa.
Aliwaagiza askari wa bandari kuhakikisha ifikapo kesho (Jumatatu) saa 6:00 mchana majina ya askari wa kampuni ya ulinzi wanaolinda boya hilo waliotumika kuiba yanakuwa kwake.
Alisema inaonekana askari hao wa kampuni inayolinda wanahusika kutokana na wiki iliyopita ilipobainika wizi huo walikurupushwa wabadhirifu hao na kukimbia kisha kuangusha bunduki.
“Ni dhahiri wanaofanya wizi huu ni wataalamu, kwani wanafungua na kufunga kitaalamu, jambo ambalo mvuvi wa kawaida hawezi kutokana na kuhitaji kukaa chini ya maji kwa saa sita,“ alisema.
Mwakyembe alisisitiza kuwa baada ya kubainika kwa askari waliohusika watafunguliwa kesi ya kuhujumu uchumi, kwani boya hilo lilijengwa kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 60 (Sh bilioni 97.8) ambazo ni mkopo na bado serikali haijaanza kuulipa.
Pia aliitaka Kampuni ya Kimataifa ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER) kama wanataka suluhu na serikali kuvunja mkataba na kampuni hiyo ya ulinzi inayotuhumiwa kwa wizi huo kuanzia kesho.
“Ninachotaka ni kumfahamu aliyewatuma na kumchukulia hatua huku kampuni ile ya ulinzi Jumatatu (kesho) ilete picha zote za walinzi waliokuwa zamu siku ile ili tulipie kwa kutoa magazetini kwa nia ya kuwatafuta,” alisema.
Alisisitiza kuwa, pia atahitaji picha za walinzi wote waliokuwa wakilinda boya ili baada ya upelelezi kukamilika wawekwe hadharani.
Aidha, Mwakyembe aliwapongeza wafanyakazi wa bandarini kwa kazi nzuri wanayofanya sasa, licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa na kubainisha kuwa utatuzi umebaki katika bodi, kwani kuna mpasuko.
Alisema haiwezekani kuendelea kuangalia yeye ana ‘saruji’ kali ya kuziba mpasuko huo na atafanya hivyo kabla ya kesho kwani ni sababu ya kuzorotesha utendaji kazi wa bandari.
“Udokozi sasa umepungua hadi baadhi ya nchi kama Zimbabwe wamepongeza, sasa mpasuko huu wa bodi nitaumaliza mapema na kuanzia sasa katika bodi hiyo kutakuwa na mjumbe mmoja ambaye ni mwakilishi wa wafanyakazi ili kuwawakilisha,” alisema.
Waziri huyo pia alisema kuanzia sasa ni marufuku kupeleka boti au meli kutengenezwa Mombasa nchini Kenya na ikishindikana kufanyiwa matengenezo bandari ya Dar es Salaam, basi waombe kibali kwake au kwa katibu mkuu wa wizara ya uchukuzi ili kusaidia katika kuomba jeshi kutengeneza, kwani ni aibu kuendelea kupeleka Mombasa.
Pia aliagiza muundo wa ajira kwa wafanyakazi wa bandari uwe umekamilika kufikia mwisho wa mwaka huu na kuhakikisha vibarua waliokaa muda mrefu wanaajiriwa katika nafasi walizopo na siyo kupelekwa waajiriwa wapya.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Madeni Kipande alisema kutokana na maelekezo ya Waziri Mwakyembe aliyoyatoa Desemba mwaka jana wameweza kuongeza posho kwa wafanyakazi za usafiri kuwa Sh 200,000 na chakula Sh 100,000 pamoja na kuongeza malipo ya kufanya kazi muda wa ziada.
No comments:
Post a Comment