Askofu Telesphor Mkude. |
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude, amesema ili amani iendelee kudumu ni vema kila mtu akajua haki na mipaka yake kwenye jamii ili kuepuka mifarakano isiyo ya lazima.
Hivyo ameiomba Serikali kuendelea na juhudi zake katika kuhakikisha amani iliyopo nchini inadumishwa na kulindwa.
Askofu Mkude alitoa ushauri huo juzi, baada ya kuzindua Kanisa la Mchungaji Mwema Sokoine katika Kijiji cha Wami-Sokoine wilayani Mvomero, Morogoro.
Sokoine (Edward) alikufa kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984 eneo la Wami Luhindo, katika barabara kuu ya Dodoma - Morogoro, kilometa 40 kutoka mjini Morogoro wakati akitoka bungeni Dodoma kwenda Dar es Salaam akiwa Waziri Mkuu.
Uzinduzi wa Kanisa hilo ulihudhuriwa pia na familia ya Sokoine kutoka wilayani Monduli na baadhi ya maaskofu wa majimbo ya Kanisa hilo nchini.
Kanisa la Mchungaji Mwema Sokoine limejengwa kwa zaidi ya Sh milioni 200 likiwa chini ya Parokia ya Dakawa kwa lengo la kumuenzi Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyeacha sifa ya kuwa mchapakazi hodari na mtetezi wa wanyonge.
Kwa mujibu wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa dini wana jukumu la kuhakikisha amani inaendelea kuwepo.
Hata hivyo, alitolea mfano wa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwapo kwa muda katika Wilaya ya Mvomero, inatokana na watu kushindwa kujua haki zao na pia kushindwa kuheshimu mipaka yao.
"Serikali iendelee na juhudi zake za kudumisha amani na ikibidi tukutanishwe mara kwa mara watu wa imani tofauti ili kujadili masuala ya amani na kuyawekea mikakati," alisema Askofu Mkude.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, alilishukuru Kanisa hilo kwa kutoa ushirikiano kwa Serikali katika masuala ya maendeleo.
"Tunashukuru kwa ushirikiano wa madhehebu ya dini katika kukomboa wananchi kielimu, kiafya na masuala mengine ya maendeleo, hakika Serikali iko pamoja nayo," alisema Mkuu wa Wilaya hiyo.
Kwa upande wao wananchi wa jamii ya wafugaji wa Kimasai katika Kijiji cha Wami-Sokoine, waliliomba Kanisa hilo kupanua wigo wa ufadhili kwa watoto wa jamii ya Kimasai, kwani wamekuwa nyuma kielimu kwa muda mrefu.
Akisoma risala ya wananchi hao, Joshua Lugasu alisema wanalishukuru Kanisa kwa kufadhili elimu ya msingi, sekondari na vyuo kwa wanafunzi 25, lakini bado mahitaji ni makubwa.
No comments:
Post a Comment