WENYE MABASI 'WAMPIGA STOP' MNYIKA SAKATA LA WAPIGADEBE...

John Mnyika.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (TABOA) kimemtaka Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kutoingilia suala la uwepo wa wapigadebe katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, kwa lengo la kutoathiri shughuli za utendaji kituoni hapo.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Taboa, Enea Mrutu alipokuwa akizungumzia masuala mbalimbali, yanayohusu utendaji ndani ya kituo hicho kikubwa cha mabasi nchini.
Alisema Mnyika amekuwa akiwataka wapigadebe kutoondoka kituoni hapo hadi pale watakapotafutiwa maeneo mengine mbadala ya kufanyia shughuli zao, suala lililoikasirisha Taboa.
Alisema wakati wadau mbalimbali wa mabasi na Serikali, wakipigana kumaliza kero ya wapigadebe kituoni, si jambo la busara kwa kiongozi huyo wa kisiasa, kukwamisha kwa kutetea uwepo wao mahali hapo.
"Tunamshauri Mnyika kuliacha suala hilo kama lilivyo, hatuna nia mbaya na malengo yake, isipokuwa tunamtaka kutambua kuwa hatutaki uwepo wa wapigadebe kituoni Ubungo, kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kusababisha kero kwa abiria," alisema Mrutu.
Aidha, Taboa kupitia kwa Katibu hiyo, kimeliomba Jeshi la Polisi kufanya mabadiliko ya askari katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo ili kukomesha mahusiano, yanayojitokeza kati ya askari hao na baadhi ya watendaji mbalimbali katika sekta ya usafiri wa mabasi kituoni hapo.
Alisema wapo baadhi ya askari, wamedumu zaidi ya miaka kumi kituoni hapo, hivyo kuwa na mahusiano yanayochangia uwepo wa vitendo vya rushwa.

No comments: