Kilontsi Mporogomyi. |
Mwanasiasa mkongwe nchini aliyepata kuwa Mbunge wa Kasulu Magharibi kwa miaka 10 na Naibu Waziri wa Fedha enzi za utawala wa Rais Benjamin Mkapa, baada ya kipindi kirefu cha ukimya, sasa ameachana na siasa, amegeukia kumtumikia Mungu kama Askofu Mkuu.
Kilontsi Mporogomyi kwa sasa ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Muujiza, Uponyaji, Kufunguliwa na Utajirisho, ambalo lipo Makongo Juu, Dar es Salaam na linahubiri utajiri wa hekima ya Neno la Mungu, fedha na afya na linalopinga umasikini kwa kigezo cha wokovu.
Katika mahojiano maalumu na mwandishi wiki hii, Askofu Mkuu Mporogomyi alisema anafurahia kuwa mtumishi wa Mungu, kwa kuwa hajawahi kujutia safari ya kumtumikia Mungu aliyoianza mwaka 2006 na kutimia 2009, lakini anakerwa na namna umasikini unavyoendelea kulitafuna Taifa wakati uwezo wa kupambana nao upo.
Alisema katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo, maono yake ni kuwa na waumini wenye uchumi mkubwa ambapo anajiandaa kufungua miradi ya kiuchumi itakayowezesha waumini kujipatia kipato.
Alisema sasa anajiandaa kuendesha harambee ya ujenzi wa kanisa jipya Oktoba, sehemu kubwa ya fedha za ujenzi ikitoka kwake na waumini kwa hiari kupitia ‘kupanda mbegu’.
Mwanasiasa huyo mkongwe, alisema njia pekee ya Tanzania kumaliza tatizo sugu la umasikini ni kuweka mkazo katika kukusanya kodi na kuondoa msamaha wa kodi kwa baadhi ya kampuni kama za simu, madini na mafuta, ikiwa ni njia pekee ya kuongeza mapato ya nchi.
Aidha, alishauri serikali ipange mkakati wa wazi wa kuwezesha wawekezaji wazalendo badala ya kuelekeza nguvu kubwa kwa wageni.
“Tunaweza kuiga mfano wa nchi za wenzetu, kwa mfano Afrika Kusini, wameamua kuweka sera za kuinua wawekezaji weusi kwanza, suala hili lipo wazi, tuache dhana kwamba mtu mweusi hawezi, nani kasema hili?
“Serikali ijenge mazingira ya kuinua watu wake kuwekeza ili fedha zibaki nchini na kuendeleza uchumi wa ndani badala ya kubebwa wote na wawekezaji wa kigeni ambao asilimia kubwa ya faida inakwenda kujenga kwao,” alisisitiza Askofu huyo ofisini kwake mtaa wa Indira Gandhi.
Alisema haikuwa rahisi kuacha siasa na kufanya kazi ya Mungu ingawa hata wakati akiwa Mbunge, alikuwa Mchungaji wa Kanisa hilo ambalo sasa ni Askofu Mkuu.
Alisema sauti ya Mungu kumwita aliisikia kupitia mgonjwa aliyemwombea India, alikokwenda kutibiwa baada ya kupooza baadhi ya viungo vya mwili na kulazimika kufanyiwa operesheni zaidi ya mara tano.
“Mgonjwa nilimwombea apone saratani, akiwa kitandani hajiwezi, kwa maombi yangu alikaa na kuzungumza nami kimwujiza, nilianza kumwona Mungu, mgonjwa yule ni miongoni mwa wengi nilioombea wakapona katika Hospitali ya Apollo.
“Yeye alipoongea nami aliniambia Mungu ameweka huduma ya kuombea watu ndani yangu na nikirejea Tanzania natakiwa kuifanya, nilitii na ndiyo sababu naifanya, nimemwona Mungu katika huduma hii,” alisisitiza Askofu huyo.
Alisema, yeye na waumini wake wapatao 150 wa Dar es Salaam, wanaamini katika uzuri wa fedha na wala fedha si dhambi kama baadhi ya viongozi wa kidini wanavyohubiri, alisema bila fedha huduma ya Mungu haisongi mbele na kubaki kuombaomba, ukiwalazimisha waumini ambao ni masikini, nao watoe hata wasivyonavyo, wengine wataishia kuiba ili wamridhishe Mchungaji.
Alisema yeye anatoa sehemu ya mali na fedha zake kusaidia wahitaji na anakiri kutokana na huruma yake katika kutoa, kusaidia watu kutatua matatizo yao kwa kufungua miradi, kuwafadhili kwa mikataba rasmi, na alipata kutapeliwa fedha zinazokaribia Sh bilioni moja na kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, alisamehe akijua atapata zaidi ya hizo.
Alisisitiza kusikia baadhi ya wabunge kuwa na mabilioni ya fedha, wengine kuzihifadhi nje huku akikiri kwamba wakati akiwa mbunge, akitokea Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuwa Mshauri wa Masuala ya Uchumi akiiwakilisha Tanzania, hakuishi maisha ya ubunge kwa starehe kutokana na kipato alichokuwa akipata, kuwa kidogo kuliko mahitaji jimboni mwake.
“Mbunge au waziri mwenye fedha nyingi ameiba, ubunge si fedha, ni karaha ikiwa kweli umeitwa kutumikia, ni lazima uwe tayari kuchangia ujenzi wa madarasa, zahanati, barabara, madaraja na majanga yatakayotokea jimboni, achilia mbali watu wanaokuja binafsi kuomba msaada mpaka nyumbani kwako, utakuwa tajiri kivipi?” alihoji Baba Askofu Mporogomyi.
Akizungumzia hali ya Bunge sasa, alisema baadhi ya watu hawana maadili, wanafanya Bunge mahali pa vurugu, anakiri nidhamu kushuka, hivyo anashauri kanuni ziboreshwe na kurejesha heshima ya Bunge, akiongeza kuwa wapo vijana wenye akili bungeni, wanaopaswa kupewa nafasi kudhihirisha uwezo wao kwa Taifa.
No comments:
Post a Comment