Baadhi ya dawa za kulevya zilizokamatwa hapa nchini. |
Watanzania 247 wamekamatwa katika nchi mbalimbali duniani na wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha dawa za kulevya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William Lukuvi, alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).
Katika swali hilo, Magige aliitaka Serikali ieleze ukubwa wa biashara ya dawa za kulevya nchini na ukoje na kuhoji kama haioni kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo kwenye viwanja vya ndege wanakopita watuhumiwa.
Mbunge huyo pia aliitaka Serikali, ieleze imefanya juhudi gani za kukabiliana na hali ya upitishwaji wa dawa hizo.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo nchini, unadhihirishwa na idadi hiyo ya watuhumiwa Watanzania wanaoshikiliwa nje ya nchi kuanzia 2008 hadi Julai 2013.
Mbali na Watanzania hao nje ya nchi, Lukuvi alisema nchini kuna wageni wapatao 31 wanaoshikiliwa mahabusu katika magereza ya Keko na Ukonga.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), aliomba kuuliza swali la nyongeza ambapo aliitaka Serikali kutaja kwa majina wahusika katika biashara ya dawa za kulevya.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema kazi ya Serikali si kutaja majina, bali kuyapokea na kuyafanyia uchunguzi na mwisho kuchukua hatua za kisheria.
“Si kazi ya Serikali kutaja wahusika bungeni, lakini tunachofanya kwa ambao wanatajwa ni kuwapeleka katika vyombo husika na kuendelea na uchunguzi na wakithibitika ndipo wanatajwa na kuchukuliwa hatua.
“Tukisema tuwataje, hata humu ndani wabunge wote watakwisha maana wako kwengi wanaotajwatajwa. Hata gazeti la Jamhuri limetaja maana wenzetu wanao ushahidi nao, na wale wasioridhika wanaweza kwenda kushitaki. Hivyo walio na majina na vielelezo watuletee ili tuwashughulikie.
Baadhi ya wabunge walionekana kuguna na kuzomea pale Lukuvi alipokuwa akitoa ufafanuzi wa suala hilo, jambo lililomfanya Spika Anne Makinda, kukemea hali ya zomeazomea ndani ya Bunge.
Hivi karibuni, vita dhidi ya dawa za kulevya, imekuwa gumzo baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuapa kuzuia uchochoro wa kupitisha dawa hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kwa kuanzia, Dk Mwakyembe alitaja maofisa alioagiza wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashitaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya, kwa tuhuma za kupitisha dawa za kulevya katika uwanja huo.
Maofisa hao ni pamoja na Maofisa Usalama, Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana.
Mbali na maofisa hao, pia aliagiza Jeshi la Polisi kumwondoa mara moja katika uwanja huo, askari Polisi, Koplo Ernest na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha mabegi sita ya dawa za kulevya, yaliyokamatwa Afrika Kusini.
Pia alisema Polisi inapaswa kumsaka Nassoro Mangunga, aliyekwepa vyombo vya Dola vya Afrika Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya dawa hizo.
Dk Mwakyembe alisema mbeba mizigo katika uwanja huo, Zahoro Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashitaka, ili aunganishwe na wenzake kujibu mashitaka ya jinai.
Dk Mwakyembe pia aliiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kufikisha mbwa wakati mwafaka kukagua mabegi hayo na kuliletea Taifa fedheha kubwa.
No comments:
Post a Comment