WAKUU WAHOFIA NCHI KUTAWALIWA NA WAGENI...

Abbas Kandoro.
Wakuu wa mikoa na wilaya nchini wana hofu nchi kutawaliwa na wageni endapo baadhi ya vipengele katika Rasimu ya katiba havitabadilishwa.

Wakuu hao walisema hayo jana Dar es Salaam wakati wakitoa mapendekezo yao baada ya kupitia Rasimu hiyo.
Akisoma mapendekezo hayo kwa niaba yao huku akiwa na baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema msingi wa Katiba ni kuweka mfumo wa mustakabali wa wananchi na Taifa lao.
Akitolea mfano, alisema katika rasimu hiyo kuna kipengele ambacho kinabainisha kwamba mtoto wa miaka saba akikutwa ndani ya mpaka wa Tanzania na wazazi wake hawajulikani, tayari atahesabiwa kuwa raia wa Tanzania.
"Hali hiyo ni hatari kwa sababu mtu kutoka Taifa lolote anaweza kupenyeza mtoto wake na akawa anamhudumia kwa siri na baadaye akagombea uongozi na kuupata na akafanya mambo ambayo hatujatarajia, kwa kweli tusirahisishe uraia wetu kiasi hicho, kwa sababu baadaye hali inaweza kuwa mbaya," alihadharisha.
Alisema masuala kama ya uraia yanayogusa wananchi moja kwa moja na rasilimali zao inashauriwa Katiba itoe maelekezo ya wazi, ili Mtanzania awe mtu anayejipambanua kwa sifa za wazi, badala ya  zinazopendekezwa ambazo zinaonekana mbeleni zinaweza kusababisha utata. 
Kuhusu muundo wa Serikali wakuu hao walipendekeza wa serikali mbili kama ilivyo sasa, kwa kuwa mfumo wa serikali tatu unaonesha dalili ya rasilimali za kuendesha serikali hizo kwa kiasi kikubwa zitatoka Tanzania Bara na hivyo kuuweka Muungano katika hali tete kuhimili.
"Mapendekezo ni kuja na mikakati ya pamoja ya kukabili changamoto zilizopo za Muungano badala ya kutafuta njia ya mkato ambayo itatoa mianya ya kuvunjika kwa Muungano kinyume na lengo zima la Katiba Mpya la kuulinda," alisema.
Kwa upande wa masuala ya kisheria walipendekeza Katiba ambayo ni sheria mama iundwe ili kutoa matamko ya msingi ya haki na wajibu wa wananchi, viongozi na vyombo kwa mustakabali wa wananchi na Taifa kwa jumla.
"Ibara nyingi kwenye Rasimu zinatoa ufafanuzi mrefu ambao ungetakiwa kufanywa katika sheria  zinazofuatia tamko la kikatiba, kwa mfano suala la haki za binadamu na miiko/maadili ya viongozi, inapendekezwa yatolewe tamko la msingi kwenye Katiba na kuachia sheria zilizopo na zitakazotungwa kuchukua nafasi yao," alisema.
Kwa upande wa tunu na alama za Taifa walipendekeza Mwenge wa Uhuru ambao upo karibu katika kila alama za nchi ukileta matumaini, mshikamano na kuhamasisha maendeleo, uongezwe katika alama kuu za Taifa pamoja na Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Nembo ya Taifa.
Katika tunu za Taifa walipendekeza kuongezwa tunu ya Amani na Utulivu ambayo wanaamini ndiyo msingi mkuu wa shughuli zote binafsi na za pamoja katika kufikia malengo ya kimaendeleo.
Kwa upande wa wajibu na haki za raia wakuu hao walipendekeza msingi mkuu wa kudai haki utanguliwe na wajibu ili kama Taifa ujengeke utamaduni wa kuwajibika ambao utachochea maendeleo ya kasi na utii wa sheria kuanzia ngazi ya mtu binafsi, jamii na taasisi.

No comments: