Baadhi ya abiria waliokuwa wakitarajia kusafiri kwa treni ya TAZARA wakiwa hawajui hatima yao kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa shirika hilo jana. |
Wafanyakazi 1,067 wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), wamefukuzwa kazi mara moja kuanzia jana.
Tamko hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Ronald Phiri.
Alisema wafanyakazi hao wamefukuzwa kazi na utumishi wao hautakiwi tena. Alisema TAZARA itatangaza nafasi za kazi kwa ajili ya nafasi zote zilizo wazi na kuajiri tena wale tu wenye sifa.
"Wafanyakazi hao waliendesha mgomo usio rasmi. Sisi tulikuwa tayari kufanya nao mazungumzo, lakini wao walikataa wakidai mpaka watakapolipwa mishahara yao ya miezi minne. Pia tuliahidi tungewalipa mishahara yao ifikapo Agosti 29, mwaka huu, lakini bado waliendelea kugoma", alisema Phiri.
Mkurugenzi huyo alisema mgogoro huo ni wa muda mrefu; na umesababishwa na kukosekana kwa mtaji wa kuendesha TAZARA.
Alisema serikali za Tanzania na Zambia, ziliahidi kutoa fedha za kulipa wafanyakazi hao hadi Agosti 29, lakini wafanyakazi hao hawakusikiliza ahadi hiyo.
Phiri alisema kutokana na mgomo huo, safari zote za treni za abiria na mizigo, zimesimama, hivyo kuiingizia hasara TAZARA ya dola za Marekani 150,000 kwa siku. Alisema kwa siku nne za mgomo huo, wamepata hasara ya dola 600,000 za Marekani.
Alisema licha ya hasara ya fedha, pia mgomo huo umefanya wateja wao kukosa imani na huduma zao.
Alipoulizwa safari za treni zitarejea lini, Mkurugenzi huyo alisema hajui zitarudi lini.
Phiri alisema tatizo la kutolipa mishahara, halipo kwa wafanyakazi wa TAZARA waliopo Tanzania tu, bali lipo hata kwa wafanyazi wa TAZARA waliopo Zambia.
Alieleza kuwa wafanyakazi wa TAZARA upande wa Zambia, hawajalipwa mishahara yao tangu mwezi Mei mwaka huu, lakini hawajagoma.
Alipoulizwa juu ya idadi ya wafanyakazi waliopo katika mamlaka hiyo, alisema jumla wapo 1,388, lakini waliohusika na mgomo huo ni hao 1,067.
Wiki iliyopita, wafanyakazi hao walishinikiza kuzungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili atatue kero zao.
"Sisi wafanyakazi tusingependa mgogoro huu ufike mbali kama tungesikilizwa na kutatuliwa kero na viongozi wetu. Hatujalipwa mishahara tangu mwezi Mei mwaka huu na bado wanataka tuendelee kufanya kazi", alisema mfanyakazi mmoja na kuungwa mkono na wenzake.
Walisema wanaamini Pinda ndiye anayeweza kutatua kero zao moja kwa moja, kwani walishapeleka malalamiko yao kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
"Si kila kero waziri anaweza kutusaidia, kama hii ya mkurugenzi kutoka Zambia ukweli tunaoumia ni sisi wafanyakazi wa Tanzania. Tunataka pia sheria ibadilike ili mtu yeyote mwenye vigezo aweze kuwa mkurugenzi wa Tazara", alisema mfanyakazi huyo. Alisema madai yao ni ya msingi, kwani shirika hilo limewatekeleza
Huku akiungwa mkono wa wenzake alisema “Treni haitasafiri mpaka kieleweke. Huwezi ukalazimisha mtu aendeshe treni wakati ana mawazo ataishi vipi. Wamekalia kuunda tume ambazo wanazilipa fedha nyingi, wakati kama wangetatua matatizo yetu, haya yote yasingetokea. Tunayemtaka hapa ni Waziri Mkuu tu! Hakuna kingine.”
1 comment:
Huyo mkurugenzi ameona hasara ya shirika kukosa milioni kama mia tisa kwa siku mbili tu, ila haoni ni hasara kiasi gani wafanyakazi hao wamepata kwa fedha za mishahara yao kukaa kwa miezi hiyo yote, pia haoni ni hasara kiasi gani wafanyakazi hao wamepata kwa kutokufanya shughuli za maendeleo na uchumi kwa kukosa pesa zao, lakini pia haoni aibu katika hilo maana mishahara hiyo ilipaswa ilipwe na fidia(interest) juu maana ni mamilioni mangapi hayo, kama yamekaa benki kwa miezi yote hiyo kiasi gani kingezalishwa kwa pesa hiyo, je kingelingana na hasara ya milioni 9 walioipata kwa siku mbili au kuzidi. Ujasiri wa kuwahukumu wengine wakati matatizo na boriti unavyo wewe umetoka wapi?
Ningekuwa mimi ningeona aibu hata kuwafukuza. Mradi kama hauzalishi haimanisha waajiriwa wasile maana siyo kosa lao, ni wewe kuwa mbunifu na kuwatimizia mahitaji yao kwa njia mbadala hata mradi huo utakapoanza au utakapopata upenyo wa kimtaji na faida.
KWA KWELI HUO NI UONEVU. MIEZI YOTE HIYO HUJUI MFANYAKAZI WAKO ANAKULA NINI HALAFU ANAKUJA KUKULALAMIKIA WEWE, UNAMFUKUZA. HAKIKA MOYO WA HURUMA NA HEKIMA UMEPOTEA NDANI YA VIONGOZI WETU.
Post a Comment