VIONGOZI WA DINI SASA WAHOFIA MAISHA YA DK MWAKYEMBE...

Dk Harrison Mwakyembe.
Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, limetaka Jeshi la Polisi kumpa ulinzi  Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kutokana wa ujasiri alioonesha kupambana na dawa za kulevya.

Kutokana na ujasiri huo, Baraza hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, limempongeza Dk Mwakyembe na kusisitiza umuhimu wa ulinzi huo kwake, kwa kuwa vita aliyoanza, inaweza kuhatarisha usalama wake.
Shekhe Salum alisema hayo jana alipozungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam,  akiongeza kuwa kitendo alichofanya waziri huyo kimeonesha uzalendo, ujasiri na upendo alionao kwa Taifa, alilosema linalochungulia kaburi kutokana na dawa hizo.
Kutokana na ujasiri huo na hatari inayomkabili Dk Mwakyembe, pamoja na kutaka ulinzi wa Polisi, Shekhe Salum pia aliomba viongozi wa dini wa imani zote, kumwombea kwa uthubutu huo.
Alisema watampa ushirikiano kwa kuunga mkono juhudi anazoonesha ambazo kwa kiasi kikubwa anaamini zitarejesha heshima ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
 “Kwa dhati kabisa Baraza linataka mawaziri na viongozi nchini kuiga mfano wake, ili kuliondoa Taifa letu katika sifa mbaya ya dawa za kulevya,” alisema Shekhe Salum.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, viongozi wana uwezo mkubwa wa kujitolea kupambana na dawa hizo, isipokuwa hakuna aliye tayari kuonesha uthubutu wake, suala alilosema kwa kiasi kikubwa limechangia mapambano dhidi ya dawa hizo kutofanikiwa.
Alisema kutokana na hali hiyo, Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi ya vijana wanaoathirika kila kukicha, kutokana na matumizi ya dawa hizo, jambo alilotaka viongozi wenzake wa dini kujipanga kuhakikisha wanawasaidia kupata nafuu wale ambao tayari wameshaathirika.
Baraza hilo pia liliipongeza Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa ukaribu na mikakati inayowezesha ukamataji na udhibiti wa utumiaji wa dawa hizo nchini.
Shekhe Salum alisema kwa hali ilivyo sasa, familia moja kati ya mbili imeathirika na dawa hizo.
Kutokana na hali hiyo, alisema Taifa limeendelea kupoteza nguvukazi ya vijana kila kukicha kutokana na matumizi ya dawa hizo, akataka viongozi wenzake wa dini kujipanga kuhakikisha wanawasaidia kupata nafuu ambao tayari wameathirika.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Mwakyembe alitaja maofisa usalama wanne wa uwanja huo na watendaji wengine, wanaotuhumiwa kupitisha kilo 180 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh bilioni 6.8.
Dawa hizo zilikamatwa Julai 5 Afrika Kusini zikitoka Tanzania, kupitia JNIA.
Mbali na kutaja maofisa hao, pia aliagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), maofisa hao wafukuzwe kazi, wakamatwe na kufunguliwa mashitaka mahakamani.
Maofisa usalama hao watakaofukuzwa kazi na kufunguliwa mashitaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya   ni Yusufu Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana.
Mbali na maofisa hao, pia aliagiza Jeshi la Polisi kumwondoa mara moja katika uwanja huo, askari Polisi, Ernest na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwenye njama za kupitisha mabegi sita ya dawa za kulevya, yaliyokamatwa Afrika Kusini.
Pia alisema Polisi inapaswa kumsaka Nassoro Mangunga, aliyekwepa vyombo vya Dola Afrika Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya dawa hizo.
Dk Mwakyembe alisema mbeba mizigo katika uwanja huo, Zahoro Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashitaka, ili aunganishwe na wenzake kujibu mashitaka ya jinai.
Dk Mwakyembe pia aliiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka kukagua mabegi hayo na kulisababishia Taifa fedheha kubwa.

No comments: