UFISADI!! BILIONI 9/- ZATEKETEA BANDARI KWA VIKAO VIWILI TU VYA WAFANYAKAZI...

Bandarini Dar es Salaam.
Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, kukagua maeneo matatu ya matumizi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili kubaini mianya ya ubadhirifu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya Sh bilioni 9 kwa ajili ya vikao viwili tu kwa mwaka.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana, Kamati ilipokuwa ikipitia ripoti ya CAG ya mwaka 2011/12 kuhusu matumizi ya Mamlaka hiyo.
Akielezea hofu ya Kamati kuhusu ubadhirifu TPA, Filikunjombe alisema inatia shaka kuona Mamlaka inatumia Sh bilioni 9 kwa mwaka kwa vikao viwili vya wafanyakazi, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko hata bajeti za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
"Matumizi ya kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa vikao viwili kwa mwaka yanatia shaka, hivyo ninamwagiza CAG afanye uchunguzi kuona kama si ubadhirifu wa fedha za walipa kodi," alisema.
Aidha, alibainisha kuwa kiasi cha Sh bilioni 6.4 kilichotumika kwa mwaka huo wa fedha kutoa matangazo ya Bandari katika vyombo vya habari, nacho kinatia shaka na kuhitaji uchunguzi.
"Kamati imeridhia pia kuwa CAG akague eneo la matumizi ya Sh bilioni 10 inayoelezwa kutumika kwa safari za maofisa wa Mamlaka ndani na nje na matumizi ya Sh bilioni 30 za uendeshaji wa shughuli za Mamlaka kama kununua vifaa," alisema Filikunjombe.
Alifafanua, kuwa ripoti ya CAG inaonesha TPA imefanya ununuzi usiozingatia sheria mara nne mfululizo bila kibali cha wizara husika, jambo linaloifanya Kamati itilie shaka ununuzi huo.
Alisema wana imani kubwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, lakini pamoja na kuamini utendaji na usimamizi wake, lazima uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha katika Mamlaka hiyo ufanyike.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imemwagiza  Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara awapeleke mahakamani maofisa wa Halmashauri ya Kiteto waliotumia Sh milioni 10 za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) kwa kuwa walikosea kisheria kutumia fedha za Mbunge kwa matumizi yao.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajab Mbarouk Mohammed alisema wakati Kamati yake ikipitia ripoti ya CAG ya mwaka 2011/12 kuhusu Hesabu za Halmashauri ya Kiteto kuwa imekuwa na matumizi yanayotia shaka, hivyo kuhitaji kuchunguzwa.
"Kuna mambo mengi yanatupa wasiwasi kuhusu matumizi yenu, hasa kiasi mnachoonesha mnakusanya kutoka mazao kupitia wakala wa vyama vya ushirika.
"Sh milioni 500 inaonesha hazijapokewa na halmashauri ziko wapi? Katika rekodi ya makusanyo inaonesha wakala alikusanya kutoka mauzo sasa imekuwaje hamjazichukua? Kuna mchezo kati yenu, madiwani na mawakala, tumeliona hili tatizo na tunataka mlitolee maelezo," alisema Mohammed.
Wakati huo huo, Kamati hiyo iliipa halmashauri hiyo hadi mwisho wa mwaka huu iwe imelipa wadai na kuongeza ukusanyaji wa mapato, vinginevyo itakuwa katika hatihati ya kupanguliwa kutokana na uzembe usioheshimu matumizi ya fedha.

No comments: