Helikopta ya Polisi. |
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda, amefutiwa mashitaka ya kuhamasisha vurugu yaliyokuwa yanamkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Ponda alifutiwa mashitaka hayo na Hakimu Mkazi, Hellen Riwa baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kufuta mashitaka hayo kwa kuwa hana haja ya kuendelea kumshitaki.
Hati hiyo iliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, wakati Shekhe Ponda alipofikishwa mahakamani hapo jana asubuhi.
Ulinzi katika eneo la Mahakama ulikuwa mkali na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo, Shekhe Ponda alisafirishwa kwenda Morogoro ambako amefunguliwa mashitaka.
Shekhe huyo alisafirishwa na maofisa wa Polisi kwa helikopta ya Jeshi hilo kutoka gerezani Segerea, Dar es Salaam hadi Morogoro na kusomewa mashitaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro.Helikopta hiyo ikiwa na Ponda ilitua katika viwanja vya gofu vya Gymkhana saa 5:03, asubuhi na kupandishwa kwenye gari aina ya Land Cruiser namba T 007 BQC hadi mahakamani hapo.
Mahakamani umati mkubwa wa wananchi kutoka maeneo ya jirani wakiwamo watumishi wa ofisi za Serikali, waliacha majukumu yao na kujaa kando ya viwanja hivyo vilivyokuwa na ulinzi mkali wa Polisi wa kutuliza ghasia, askari kanzu na polisi wa kikosi cha mbwa.
Kukiwa na utulivu mkubwa ndani na nje ya Mahakama, Ponda aliingizwa ndani ya mahakama saa 5.20 kusomewa mashitaka kwa makosa anayodaiwa kufanya akiwa Morogoro.
Ponda alisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate, akiwa amekaa kutokana na kudai kuwa na maumivu ya jeraha begani.
Katika mashitaka hayo, Wakili Mkuu wa Serikali, Kanda ya Morogoro, Benard Kongola, alidai kuwa Shekhe Ponda alitenda makosa matatu Agosti 10 jioni katika viwanja vya shule ya msingi Kiwanja cha Ndege mjini humo.
Kwa mujibu wa mashitaka hayo, anadaiwa kuvunja Sheria ya Adhabu kwa kutoa kauli za uchochezi kwa jamii na kukiuka amri halali ya Mahakama.
Wakili Kongola katika tuhuma hizo za uchochezi, alinukuu maneno aliyodai ni ya uchochezi yaliyotolewa na Shekhe Ponda katika mkutano wa hadhara eneo hilo.
Shehe Ponda anadaiwa kusema: “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.
“Kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za Msikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu, muwapige sana.“
Kwa mujibu wa madai ya Wakili Kongola, kauli hiyo ya Ponda ni kwenda kinyume na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, iliyotolewa Dar es Salaam Mei 9.
Katika amri hiyo, Mahakama hiyo ilimpa Shekhe Ponda adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja, na kumtaka asifanye jambo lolote la uvunjifu wa amani na badala yake ahubiri amani.
Tuhuma za pili dhidi ya Shekhe Ponda, ni uvunjifu wa Sheria ya Makosa ya Jinai siku hiyo, alipotoa maneno ya uchochezi yaliyohatarisha kuathiri imani za watu wengine.
Shekhe Ponda anadaiwa kusema:“Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa kuua, kubaka na kutesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
“Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa
Loliondo walipokataa Mwarabu kupewa kipande cha ardhi ya uwindaji, baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”
Katika tuhuma za tatu, Shekhe Ponda anadaiwa kutenda kosa la kutoa maneno ya uchochezi kwa wananchi wakati wa Kongamano hilo lililofanyika Agosti 10 katika uwanja wa shule ya msingi Kiwanja cha Ndege, mjini humo. Ponda alikana mashitaka yote.
Upande wa Mashitaka ulimweleza Hakimu kuwa upelelezi wa kesi hiyo, umekamilika na hivyo kupendekeza siku ya kuanza kusikilizwa, ambapo Hakimu alitaja Septemba 2.
Hata hivyo, tarehe hiyo ilipingwa na mawakili wanaomtetea Shekhe Ponda;Wakili Ingas Punge aliomba kuteta na mteja wake kizimbani na kukubaliwa na Hakimu ili kupata muda utakaofaa kwa ridhaa ya Shekhe Ponda.
Baada ya mazungumzo hayo, Wakili Punge na mwenzake Bill Tarimo, walitoka na mapendekezo ya kesi hiyo kusikilizwa Agosti 26.
Walidai kuwa mteja wao anaendelea na matibabu ya jeraha na pia upande wa mashitaka umethibitisha kuwa upelekezi umekamilika, hivyo hakuna haja ya kuchukua muda mrefu.
Kutofautiana huko kwa muda wa kutajwa tena kwa kesi hiyo, kulisababisha Hakimu aamuru mawakili wa pande hizo mbili watoke nje ya Mahakama, wajadiliane na kufikiwa mwafaka wa pamoja kuhusu tarehe ya kutaja tena kesi hiyo.
Baada ya majadiliano, mawakili hao walirudi mahakamani na kupendekeza kesi hiyo isikilizwe Agosti 28 na kukubaliwa na Hakimu.
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi, upande wa mashitaka uliwasilisha ombi la kufunga dhamana kwa mshitakiwa, kwa madai kuwa Shekhe Ponda alishahukumiwa na Mahakama kutumikia kifungo cha nje na baadaye akavunja amri ya Mahakama.
Hakimu alizingatia ombi la upande wa mashitaka na kuamuru Shekhe Ponda aendeleee kukaa rumande hadi siku ya kusikilizwa tena kwa shauri hilo.
Baada ya hapo, msafara wa magari ya Polisi ulianza saa 6.30 kumrejesha Shekhe Ponda kwenye viwanja vya gofu kupanda helikopta kurejea Dar es Salaam, ambapo anatarajiwa kusomewa mashitaka mengine kama hayo, Zanzibar.
Ulinzi mkali uliimarishwa mahakamani hapo wa magari matatu aina Land Rover Defender, yakiwa na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wenye silaha, mabomu ya kutoa machozi, mbwa na pia kukiwa na gari la maji ya kuwasha huku barabara inayokatiza mahakamani hapo ikifungwa kwa muda.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya ofisi jirani na Mahakama hiyo ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya, Hazina Ndogo, Ofisi ya Madini, Ofisi ya Ukaguzi na Posta, kushindwa kuendelea na kazi na watumishi kutoka nje kushuhudia.
Kabla ya kuondolewa mahakamani hapo, waumini kadhaa wa dini ya kiislamu walisimama mbali na gari lililombeba Shekhe Ponda wakisoma Kurani kumwombea Shekhe huyo.
No comments:
Post a Comment