NDEGE YATUA KWA DHARURA NDANI YA ZIWA MANYARA...

Ndege hiyo ililazimika kutua Ziwa Manyara (pichani).
Ndege ndogo aina ya Vich Grave, imelazimika kutua majini katika Ziwa Manyara kwa dharura, baada ya kupata hitilafu na kushindwa kutua katika viwanja vya ndege.

Kutokana na dharura hiyo, abiria sita iliyokuwanao wakitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam kupitia Zanzibar, waliokolewa kwa mitumbwi ya wavuvi na kukimbizwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, kwa helikopta kwa matibabu.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliyekuwa  eneo la tukio, alisema ilianza safari jana saa 12.58 asubuhi na kupata hitilafu ikiwa angani saa 2.43 asubuhi eneo la Iambi, Kusini mwa wilaya ya Babati.
“Ni kweli ndege imeanguka Ziwa Manyara na hakuna kifo bali watu wamepata majeraha… siwezi kusema ndege imeharibika kwa kiasi gani, tunasubiri wataalamu wa ndege wafike eneo hili waivute,” alisema Kamanda Sabas.
Abiria sita waliokuwa kwenye ndege ni Anik Kashasha (51), Regina Mutabihirwa (58), Alois Mwanga (60), Naburi Meeda (80), Ashura Mohamed (38) na Protas Ishengoma (45), wote wakazi wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, abiria hao walitibiwa na wataendelea na safari yao kwa usafiri mwingine wa ndege.  Rubani aliyetajwa kwa jina la Kondo (51) hakudhurika kwenye ajali hiyo.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda alisema rubani awali alitaka kutua uwanja mdogo wa Arusha, lakini akaona hatafika, akajaribu  kuelekeza ndege itue uwanja mdogo wa Manyara, lakini pia akaona haitafika, ndipo alipoona eneo salama la kutua bila madhara makubwa ni Ziwa Manyara.
Dharura ya ndege hiyo imekumbusha ajali mbili za ndege zilizotokea Arusha hivi karibuni. Ajali ya kwanza ni ya mfanyabiashara maarufu, Babu Sambeki aliyeanguka na ndege yake, wakati akijaribu kutua uwanja mdogo wa Arusha na kufa baada ya kuparamia mti.
Nyingine ni  ya ndege ya madaktari ya Kanisa Katoliki, ambayo ilianguka na kujeruhi abiria saba, wakiwamo marubani wawili muda mfupi baada ya kuruka katika kiwanja kidogo cha ndege kijijini  Merugwayi wilayani Longido, Arusha.

No comments: