MTANZANIA ACHAGULIWA KATIBU MTENDAJI WA SADC...

Dk Stergomena Tax.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amechaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Tax, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo, amepata asilimia 79 ya kura zote na amemshinda mpinzani wake ambaye Waziri wa Uwekezaji, Rasilimali na Viwanda wa Shelisheli, Peter Sinon aliyepata kura asilimia 72.
Waliopiga kura juzi ni Baraza la Mawaziri la SADC.  Tax anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Tomaz Salomao kutoka Msumbiji anayemaliza muda wake na aliyeshika nafasi hiyo kwa vipindi viwili ambavyo ni miaka minane mfululizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema Tax atathibitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi unaoanza leo na kumalizika kesho mjini hapa.
“Tunaamini atathibitishwa na sisi Tanzania tumejisikia kupewa heshima na kuaminiwa na nchi 14 zilizopiga kura na pongezi tumeshaanza kuzipokea,” alisema Membe.
Hata hivyo, baraza hilo la mawaziri la SADC limeshindwa kumpata Naibu Katibu Mtendaji kutokana na taratibu za uchaguzi kukiukwa hivyo limetoa mwezi mmoja na baada ya hapo mawaziri hao watakutana tena kwa ajili ya kumchagua naibu huyo. Alisema nafasi hiyo wanategemea kuchukuliwa na Afrika Kusini kutokana na nchi hiyo kutokuwa na watu kwenye uongozi wa SADC.
Jana Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Amani, Ulinzi na Usalama alitoa taarifa ya  masuala ya ulinzi, amani na usalama katika kipindi chake cha mwaka mmoja na kukabidhi uongozi kwa Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba.
Membe alisema baraza hilo la mawaziri pia limezungumzia juu ya kuanzishwa kwa Mahakama ya SADC ambapo mawaziri wa sheria na wataalamu wamepewa kazi ya kutengeneza muundo wa mahakama hiyo, kazi zake na sheria ya kuanzisha kwake bila kuingilia kazi za mahakama za nchi wanachama na taarifa ya mahakama hiyo itawasilishwa kwa baraza la mawaziri Aprili mwakani.
“Suala hili limechukua muda mrefu kwa sababu viongozi waliona mahakama hii inajipa madaraka makubwa na kuonekana inaweza kukataa maamuzi ya nchi,”alisema.
Wakuu wa  nchi pia watapokea taarifa ya maendeleo ya mgogoro wa kisiasa wa Madagascar na taarifa fupi ya uchaguzi wa Zimbabwe na kuongeza, “Zimbabwe taarifa itakuwa fupi kwa sababu suala lao lipo mahakamani lakini pia watapokea taarifa ya maendeleo ya wanajeshi wa Malawi, Tanzania na Afrika Kusini waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo eneo la Goma”.
Msimamo wa SADC kwa Madagascar ni Rais wa sasa Andry Rajoelina, rais wa zamani Didier Ratsiraka, Lalao Ravalomanana ambaye ni mke wa Ravalomanana kutogombea urais na kuwaachia wagombea wengine 46.

No comments: