Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Kiongozi wa Mbio hizo Kitaifa, Juma Ali Simai (kushoto) hivi karibuni. Simai na wenzake 9 wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo. |
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Juma Ali Simai (32) amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya kujeruhiwa kwenye ajali, iliyotokea kwenye msafara wa mbio za mwenge mjini hapa.
Msafara huo uliopata ajali, ulihusisha magari matano na watu wengine tisa akiwemo Naibu Meya wa manispaa ya Dodoma, Jumanne Ngede walijeruhiwa katika ajali hiyo. Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Zainab Chaula alisema majeruhi sita walitibiwa na kuruhusiwa.
Hali ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge inaendelea vizuri. Alisema alipata maumivu ya ndani akapoteza fahamu. “Tumempa dawa ili alale apumzike kutokana na mshtuko alioupata,” alisema Chaula. Hata hivyo msafara uliendelea na mbio.
Wengine waliojeruhiwa ni Charles Mamba (50), Dativa Kimolo (46), Amina Mgeni (36), Jacquline Magoti (39), Richard Mahelela (51), Zaituni Varinoi (43) na Gandule Chimponde (40) .
Katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati wa kuzungumzia ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Susan Kaganda alisema kiongozi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu.
Alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 2.45 asubuhi katika Kijiji cha Fufu Wilaya ya Chamwino, wakati msafara ukienda kwenye makabidhiano ukitoka Wilaya ya Dodoma Mjini kwenda Wilaya ya Mpwapwa.
Alisema moja ya magari kwenye msafara, lilikuta tuta huku dereva akishika breki ghafla na kusababisha magari yaliyokuwa nyuma yake, kugonga ya mbele, kutokana na vumbi.
No comments:
Post a Comment