MKE WA LIYUMBA AMPANDISHA MUMEWE MAHAKAMANI...

Amatus Liyumba.

Mke wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, Aurelia Ngowi amefungua kesi ya madai akipinga mumewe kuuza mali za familia na kumfukuza kwenye nyumba wanayoishi.

Aidha,  anaiomba Mahakama iamuru yeye na watoto wake waendelee kuishi kwenye nyumba hiyo, hadi shauri hilo litakapokwisha. Mama huyo anadai Liyumba aliwafukuza na kuweka walinzi ili wasiingie kwenye nyumba hiyo.
Kesi hiyo imefunguliwa mbele ya Hakimu Mkazi Jackline Rugemalila katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika hati ya madai, Aurelia anaiomba Mahakama iweke zuio la muda ili Liyumba asiuze mali za familia, pia asiuze nyumba iliyopo Africana Mbezi Beach, katika kiwanja namba 2232/2233 ambayo walikuwa wanaitumia kama makazi ya familia.
Aurelia ameiomba Mahakama iamuru waendelee kuishi katika nyumba hiyo wakati shauri hilo likiendelea pia mshitakiwa alipe gharama za uendeshaji wa kesi.
Katika hati ya kiapo inayounga mkono madai yake Aurelia anadai,alifunga ndoa na Liyumba mwaka 1978 mkoani Kilimanjaro na kupata watoto wanne na mwaka 1980 walianza kuishi kwenye nyumba iliyopo Africana.
Anadai waliendelea kuishi katika nyumba hiyo na baadaye waliamua upande wa nyumba waweke hoteli inayoitwa Amjen Executive pamoja na biashara nyingine zilizokuwa zinawaingizia kipato kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya familia.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo, baada ya Liyumba kutoka gerezani ambako alikuwa anatumikia kifungo, alihama nyumbani na kuanza kuuza mali mbalimbali yakiwemo magari, kiwanja cha ekari 50 kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani na kiwanja cha Tabata.
Anaendelea kudai kuwa Julai 18 mwaka huu, Liyumba aliwafukuza yeye na watoto wake na kufunga nyumba hiyo pamoja na eneo la biashara waliyokuwa wakiitegemea kwa ajili ya kupata fedha za matumizi ya kila siku kisha akaweka walinzi ambao  wanawazuia kuingia.
Aurelia anadai baada ya kufanya uchunguzi aligundua kuwa mume wake anauza mali walizochuma pamoja na kuongeza kuwa endapo mahakama haitaweka zuio atapata hasara kubwa.
Liyumba alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma, alimaliza kutumikia kifungo hicho Septemba 23 mwaka juzi.

No comments: