MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI ATIMULIWA CCM...

Nape Nnauye.
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM imeridhia kuvuliwa uanachama kwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kiembesamaki, Mansoor Yussuf Himid kama ilivyopendekezwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho Mkoa wa Magharibi Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC, Nape Nnauye kwa waandishi wa habari, ilisema hatua hiyo inatokana na Mjumbe huyo kukabiliwa na tuhuma kadhaa.
Alizijata baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama, kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na alikiuka maadili ya kiongozi wa CCM na kukana Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.
“Baada ya kujiridhisha vya kutosha na tuhuma dhidi ya Mansoor, NEC imeridhia uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi Zanzibar wa kumfukuza uanachama. Kwa uamuzi huo wa kumvua uanachama Mansoor sasa si kiongozi tena wa CCM.
Alisema kuwa Mansour hawezi kukata rufaa kwa sababu hicho ni kikao cha mwisho. 
Wakati huo huo, Nnauye alisema Nec imeteua makatibu wa mikoa watatu na wa wilaya 25 ambao watapangiwa maeneo ya kufanyia kazi baadaye.
 Akizungumzia suala la madiwani wanane wa Bukoba Mjini waliofukuzwa uanachama, alisema kikao cha Kamati Kuu kitakutana leo mjini hapa kumalizia kuhoji  viongozi na uamuzi kutolewa.
Hivi karibuni kamati ya maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, ilipitisha mapendekezo ya kumvua uanachama Mwakilishi huyo wa Kiembesamaki na Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo wajumbe wa NEC wakiwamo wabunge na wawakilishi walisema Mansoor alishindwa kulinda sera na Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa sababu alikuwa na msimamo wake wa kutetea mamlaka kamili ya Zanzibar.

No comments: