KUSHOTO: Marehemu Daudi Mwangosi. KULIA: Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akiweka shada la maua kwenye kaburi la Mwangosi. |
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), umekionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) dhidi ya kutumia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Wanahabari mkoani Iringa (IPC), Daudi Mwangosi kama mtaji wa kisiasa.
Tayari Chadema wameiandikia barua klabu ya wanahabari Iringa (IPC), kutaka washiriki kujenga mnara wa kumbukumbu katika eneo ambalo alikofia Mwangosi kwa kupigwa na bomu na mtu anayedaiwa kuwa askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani humo.
Akitoa msimamo wa UTPC juzi, Makamu Rais wa UTPC, Jane Mihanji alisema muungano hauungi mkono Chadema kutumia kifo hicho kama sehemu ya kujipatia umaarufu, kwani Mwangosi aliuawa akiwa katika kazi za uandishi wa habari na si siasa.
ÒTumesikia kuna habari kwamba Chadema wanataka kujenga mnara wa kumbukumbu katika eneo alikofia Mwangosi, sisi UTPC hatukubaliani nalo, Mwangosi hakuwa mwanasiasa, wasitumie jambo hilo kama mtaji wa kisiasa, watuachie wenyewe,Ó alisema.
Akizungumzia jambo hilo, Katibu Mtendaji wa IPC, Francis Godwin alikiri klabu yake kupokea barua ya Chadema ikiwaomba washiriki ujenzi wa mnara huo wa kumbukumbu.
Alisema Chadema ambao tayari wameanza ujenzi huo mwezi huu na kutarajia kuukamilisha Agosti 28, pia watafanya tamasha maalumu la kuchangisha fedha za kuisaidia familia ya Mwangosi.
Godwin alisema kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, uwekaji wa jiwe la msingi la mnara huo unatarajiwa kufanywa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
Kwa mujibu wa barua ya Chadema ya Jimbo la Mufindi Kusini Agosti 8, kwenda kwa Katibu Mtendaji wa IPC, inaiomba IPC isaidie fedha na ushirikiano katika ujenzi wa mnara huo kwenye kijiji cha Nyololo.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na katibu wa jimbo la Mufindi Kusini, Emmanuel Ngwalanje inaonekana uwekaji wa jiwe la msingi la mnara huo ulianza Agosti 20 na unatarajiwa kukamilika Agosti 28, ambapo chama hicho kitaendesha harambee kuisaidia familia ya Mwangosi.
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2, mwaka jana katika kijiji cha Nyololo mkoani Iringa, akiwa katika shughuli za uandishi wa habari kwenye mkutano wa kisiasa wa Chadema, na baadhi ya watuhumiwa wa tukio hilo tayari wamefikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment