Wasindikaji wa mafuta ya ubuyu mkoani Dodoma wamesimamisha uzalishaji kutokana na ukosefu wa wateja baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), kutamka kuwa mafuta hayo ni hatari kiafya.
Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, wajasiriamali wa mafuta hayo wamesema biashara hiyo sasa inasuasua kwa kukosa wateja wapya.
Hata hivyo, kwa wateja wa zamani waliopata tiba baada ya kutumia mafuta hayo kwa upande wa Dar es Salaam, wamekuwa wakinunua bidhaa hiyo kwa wingi kwa lengo la kuhifadhi wakihofia kutoyapata pindi yakipigwa marufuku.
Wasindikaji hao wameitaka Serikali kufanya uchunguzi haraka ili biashara hiyo iendelee kama kawaida, kwani ilikuwa ikitegemewa na wajasiriamali hasa wanawake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye viwanja vya maonesho ya 20 ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane), yanayoendelea mjini Dodoma, walisema kauli ya TFDA imewaathiri kiuchumi kutokana na kukosa masoko.
Neema John, ambaye ni mjasiriamali wa Ihumwa, alisema wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kauli za kupiga marufuku matumizi ya mafuta hayo kwani zimepunguza kwa kiasi kikubwa wateja.
Alisema kabla ya kauli hiyo alikuwa akipata masoko katika mikoa ya Mara, Tabora, Dar es Salaam na hata nje ya nchi.
Kwa mwezi alikuwa na uwezo wa kuuza kati ya lita 80 hadi 100, lakini sasa hawezi kufanya tena biashara kama awali kwani wateja waliobaki ni wa mafuta hayo kwa ajili ya kujipaka.
"Tangu Serikali itangaze mafuta haya yanasababisha saratani, wateja wamekimbia wengine hata ukiwapigia simu hawapokei," alisema mjasiriamali huyo ambaye anadai alikopa Sh milioni mbili katika Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos), kwa ajili ya kununua malighafi.
Lakini amejikuta akipata hasara kutokana na biashara kutofanyika, jambo lililomlazimu kuomba msaada kwa ndugu zake kulipa mkopo.
Hata hivyo, alisema wanashangazwa na TFDA kutamka kuwa mafuta hayo ni hatari wakati wakazi wa Dodoma wamekuwa wakitumia mbegu za ubuyu wakizitwanga na kuunga mboga tangu enzi na enzi bila madhara.
Mjasiriamali wa Kondoa, Amina Nyange, alisema alikuwa akijipatia Sh milioni 1.2 kwa mwezi kutokana na kuuza mafuta hayo, lakini baada ya kutangazwa kuwa ni hatari kiafya, ameamua kuacha.
Alisema hata kwenye maonesho hayo ameleta bidhaa nyingine, kwani hatapata soko kutokana na kauli ya Serikali kuwa mafuta hayo ni hatari.
Halima Mtaita pia wa Kondoa alisema alikuwa na uwezo wa kuzalisha lita 20 za mafuta hayo kwa mwezi, lakini mpaka sasa ana lita 100 za mafuta hayo ambayo hajui wa kumuuzia.
"Nitayauza wapi wateja wamegoma kuyanunua, nimeathirika sana kiuchumi, kwani nilikuwa na uhakika wa kupata Sh 800,000 kwa mwezi," alisema na kuongeza kuwa alikuwa akiuza lita moja ya mafuta hayo kwa Sh 40,000.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wasindikaji wa Mafuta ya Alizeti (Tasupa), Ringo Iringo, alisema wanachofanya ni kutafuta teknolojia ambayo itawawezesha wajasiriamali wadogo kusindika mafuta salama kwa wateja.
Alisema watu wengi wamejiajiri kusindika mafuta ya ubuyu, lakini tatizo ni teknolojia inayotumika kuyafanya yawe salama.
Alisema mpaka sasa hawajapata taarifa ya kisayansi kuwa mafuta hayo yanaleta saratani kwani hata wagonjwa wa kansa ya ngozi walikuwa wakitumia mafuta hayo.
"TFDA itoe mwongozo jinsi ya kusindika mafuta hayo, kwani hapa Dodoma mjini kuna wasindikaji wanaofahamika 20 mbali na walioko wilayani lakini kabla ya kutupa mwongozo wameamua kupiga marufuku.
Kwa upande wa wajasiriamali wa mkoani Dar es Salaam ambao biashara yao kubwa ni ya bidhaa zinazotokana na ubuyu yakiwemo mafuta, sabuni, unga wa ubuyu pamoja na majani yake ambao wanatarajia kwenda kuonesha bidhaa hizo katika nchi za Kenya na Uganda baada ya kuwa washindi katika shindano la fanikiwa kibiashara linaloendeshwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) walisema kwa sasa soko la mafuta hayo limeshuka kwa wateja wapya.
Wakizungumza na mwandishi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kibby General Supply anayefanya biashara ya mazao ya ubuyu, Kibibi Japhary alisema tangu kutangazwa kwa biashara hiyo mauzo kwa wateja wapya yameshuka sana kwa hofu ya kupata kansa.
"Suala hili limeleta utata na kushusha soko kwani lilitangazwa wakati wa maonesho ya Sabasaba ambapo nilikuwa nimeuza kwa mama Salma Kikwete na Mke wa Mfalme Mswati wa Swaziland walipotembelea banda letu na kuahidi wengi kuja kununua lakini baada ya kutangazwa sikupata tena wateja," alisema.
Alisisitiza kuwa kwa sasa wateja walio nao ni wale waliokwishayatumia na kupata mafanikio ambao kwa kuhofia kupigwa marufuku au kupotea wananunua kwa wingi kwa ajili ya dawa.
Mjasiriamali wa Kampuni ya Tree of Life, Jessca Lewycky alisema bado anapata wateja wa bidhaa hiyo lakini siyo kwa wingi kama ilivyokuwa hapo awali.
Alitaka TFDA kueleza kiwango kinachotakiwa kunywewa cha mafuta hayo ili watu wasipate madhara kwani dawa yoyote ikizidishwa lazima ilete madhara.
Alisema mwaka jana alienda nchini Canada na kukuta kuna utafiti wa bidhaa za ubuyu anazotengeneza yeye ambayo imeonesha kutokuwepo kwa tindikali inayoelezwa kuwepo na kuleta madhara.
Alisema alitaka serikali kuangalia mbele zaidi kwa faida ya mafuta hayo kuliko madhara kwa kuangalia namna ya kuwasaidia watanzania kwani mbegu ya ubuyu ni pekee yenye omega za aina tatu zenye manufaa kwa afya ya binadamu.
"Kinachonishangaza ni kushikilia madhara ya mafuta haya wakati kuna vitu vyenye madhara kama sigara lakini vimeachwa kwa miaka mingi," alisema.
Kutokana na utata wa usalama wa mafuta hayo, tayari serikali imeamua kuyafanyia utafiti na hivi karibuni itatoa tamko la kumaliza gumzo hilo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando, aliliambia gazeti hili kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za utafiti huo, na muda si mrefu itatoa msimamo ili kuondolea wananchii utata.
"Tumeona kila mtu anazungumzia usalama wa mafuta ya ubuyu, lakini siku chache zijazo tutawaita na kutoa msimamo wa Serikali ili kuwaondolea wananchi utata uliopo wa kila mtu kusema lake," alisema Dk Mmbando.
Utata kuhusu usalama wa mafuta ya ubuyu, ulianza mwezi uliopita baada ya TFDA, kueleza kuwa mafuta hayo si salama kunywewa, kwani yana tindikali inayosababisha saratani.
Kauli ya TFDA, iliungwa mkono na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, iliyoweka wazi kuwa haitambui mbegu za ubuyu kuwa zinatoa mafuta ya tiba, isipokuwa inatambua tiba inayotokana na mti huo ni majani, magome na unga.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Mbadala wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paulo Mhame, alisema Serikali haitambui mafuta ya ubuyu kama tiba.
Hata hivyo, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ilitangaza kuwa mafuta hayo ni salama yakitumiwa vizuri.
Daktari Bingwa wa Udhibiti wa Saratani wa taasisi hiyo, Dk Crispin Kahesa, alinukuliwa akisema hadi sasa hakuna utafiti wowote wa kitaalamu, uliopata kufanywa na kuonesha kuwa mafuta hayo ni chanzo cha saratani ya ini.
"Mafuta ya ubuyu si dawa bali yanazuia maradhi sugu yasiyoambukiza, ikiwamo saratani kwa sababu kitaalamu yana 'anti oxidant' (uchachu) ambayo pia hupatikana kwenye baadhi ya matunda kama maembe, machungwa na mananasi.
"Tofauti iliyopo, ni kwamba mafuta hayo yana anti oxidant nyingi tofauti na iliyomo kwenye matunda. Anti oxidant husaidia kukinga maradhi ambayo mengi si ya kuambukiza - maradhi sugu kama vile saratani, kisukari na shinikizo la damu," alikaririwa Dk Kahesa.
Kazi nyingine ya anti oxidant mwilini ilitajwa kuwa ni kuondoa sumu na kusaidia kutengeneza chembechembe hai mwilini.
"Narudia, mafuta ya ubuyu hayana madhara yakitumika vizuri, bali madhara ambayo watu wanayasema, yanatokana na jinsi wanavyoyatumia, kwani wajasiriamali wanaoyatoa hawajui ni mgonjwa gani anapaswa kuyatumia na kwa wakati gani," alikaririwa Dk Kahesa.
Kutokana na tamko hilo, pia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, wiki hii alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali, hivyo wananchi waamue kuyatumia au kutoyatumia.
"Tayari chombo cha Serikali ambacho kina mamlaka juu ya hili kimeshatoa tamko, hivyo ni hiari ya wananchi kuamua kuyatumia au kuacha.
"Kwa sababu ni sawa na sigara, tumesema kabisa sigara inasababisha saratani na matatizo mengine, tukaweka na onyo kwenye kasha la sigara, hivyo ni hiari kutumia au kutotumia," alisema.

No comments:
Post a Comment