BASI LAPINDUKA LIKIWA NA ABIRIA WAPATAO 80 TABORA...

Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete ambako majeruhi wamelazwa.
Watu 28 wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete huku wanne kati yao, hali zikiwa mbaya, kutokana na kujeruhiwa katika ajali ya gari.

Basi aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Ladack, linalodaiwa kuwa na abiria wapatao 80, lilipata ajali jana asubuhi wakati ikitoka Kata ya Goweko wilayani Uyui kwenda mjini Tabora.
Majeruhi walifikishwa hospitalini saa 3 asubuhi, muda mfupi baada ya kuokolewa na wenzao waliokuwa ndani ya gari hilo.
Ofisa Muuguzi wa hospitali hiyo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwa madai si msemaji, alisema  hali ya majeruhi wanne ni mbaya, lakini wengine wanaendelea vizuri.
Majeruhi ambao hali zao ni mbaya ni Mathayo Bernard,  Kashola Sazia,  Kayanga Ngeleja na mwingine aliyetambulika kwa jina la Yasini.
Akizungumza hospitalini hapo, majeruhi Bernard alisema ajali hiyo ilitokea saa 12:15 asubuhi, muda mfupi baada ya kuondoka Noweko. Alisema kabla ya basi kukosa mwelekeo na kupinduka,  walisikia kishindo .
Kwa mujibu wa Polisi mkoani Tabora, basi hilo ni lenye namba za usajili T 918 ALG, mali ya kampuni ya Ladack.
Taarifa ya polisi ilisema  dereva wake ambaye jina lake halijafahamika, alikimbia baada ya ajali hiyo na anasakwa.

No comments: