WASEMA MISHAHARA MIPYA YA WATUMISHI WA NDANI HAITEKELEZEKI...

Baadhi ya watumishi wa ndani wakiwa katika moja ya semina waliyoandaliwa.
Baada ya Serikali kuweka kisheria mshahara wa kima cha chini kwa watumishi wa ndani, Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hoteli, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU), kimeeleza kuwa utekelezaji wa sheria hiyo ni mgumu.

Akizungumza na mwandishi wiki iliyopita kuhusu sheria hiyo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Wilfred Mshana, alisema itakuwa ngumu kutekeleza sheria hiyo, kwa kuwa utaratibu wa kubaini kama watalipwa au la ni mgumu.
"Watumishi wa majumbani wanatumika kama ndugu wa waajiri... wanapachikwa majina ya udugu wakihusisha shangazi, mjomba na mengineyo, ili wakwepe kuwalipa maslahi bora na kuingia nao mikataba," alisema Mshana.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wafanyakazi wote wa ndani walioajiriwa, mbali na wanaofanya kazi za ndani kwa makubaliano mengine yasiyo ya ajira, kama muda mfupi na kuacha, wanapaswa kulipwa si chini ya 40,000/- hadi 150,000/- kwa mwezi.
Katibu Mkuu wa Chodawu, Said Wamba, alisema Chodawu wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha watumishi wanapata haki zao, lakini hiyo ni kwa wanaopeleka malalamiko kwenye chama hicho.
Alisema wanashindwa kuwafikia watumishi wote sehemu zao za kazi, kwa kuwa wengi wao hufanya kwenye nyumba binafsi, ambazo kisheria hawawezi kuingia kubaini kama kuna madhila dhidi ya mtumishi, hadi pale anapotoa taarifa.
"Kuna ugumu wa kuingia kwenye nyumba ya mtu binafsi kukagua au kufahamu kama mtumishi wa ndani ananyanyaswa au kunyimwa haki yake, hadi pale matatizo yanapokuwa makubwa na kuripotiwa kwetu," alisema Wamba.
Alisema wenye mamlaka ya kisheria ya kuwapa kibali cha kufanya hivyo, ni Idara ya Kazi Kitengo cha Ukaguzi, katika Wizara ya Kazi na Ajira, lakini inavyoonekana jambo hilo halitekelezwi.
Alitaka watumishi wa ndani, kutoogopa kudai haki yao pale wanapoona mambo hayaendi inavyostahili na ikiwezekana watoe taarifa kwenye uongozi wa serikali za mtaa kwa hatua zaidi.
Akizungumza na mwandishi, kama wafanyakazi wa kipato cha chini watalipa mshahara huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Nicholas Mgaya, alitaka wafanyakazi wasioweza kulipa mshahara huo, wasiajiri watumishi wa ndani.
Hata hivyo, Mgaya alituhumu waajiri wengi kwa kutokuwa wakweli katika kuelezea faida na hasara wanazopata, na kusababisha kima cha chini cha kisekta kupangwa isivyo na wao kubaki na faida kubwa.
Kwa mujibu wa tangazo la Serikali lililoainisha kima cha chini kwa sekta binafsi, ikiwemo kada ya watumishi wa ndani, zilizoongoza kwa kuwa na kima cha chini cha mshahara, ambacho ni kikubwa kwa mwezi, ni sekta ya mawasiliano ya simu, huduma za kifedha, migodi iliyothibitika kuwa na madini, na kampuni za kimataifa za nishati ambazo kima cha chini ni Sh 400,000 kwa mwezi.
Sekta zinazofuata kwa kuwa na kima cha chini chenye mshahara mnono kwa mwezi ni ya ujenzi kwa kampuni za ujenzi za daraja la kwanza, ambayo kima cha chini ni Sh 325,000.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wafanyakazi katika usafiri wa anga,   kampuni za upakiaji na upakuaji mizigo na zinazotafuta madini, kima cha chini kinapaswa kuwa Sh 300,000.
Watumishi katika kampuni za ujenzi daraja la pili mpaka la nne, watalipwa si chini ya Sh 280,000, wakifuatiwa na watumishi wa  kampuni za ujenzi daraja la tano mpaka la saba na wa hoteli za kitalii ambao kwa mwezi kima cha chini kimetajwa kuwa Sh 250,000.
Kwa wafanyakazi wa kampuni za usafirishaji za majini na nchi kavu, wakiwemo madereva na makondakta wa daladala na kampuni za uvuvi, kima cha chini kitakuwa Sh 200,000.
Wafanyakazi katika kampuni za habari, posta na usafirishaji wa vifurushi na kampuni za kimataifa za ulinzi, kampuni ndogo za kuzalisha nishati na hoteli za kati, kima cha chini kitakuwa Sh 150,000, kikifuatiwa kwa karibu na kima cha chini kwa shule binafsi za sekondari mpaka chekechea, ambacho ni Sh 140,000.
Katika sekta ya afya, kima cha chini kitakuwa Sh 132,000, kikifuatiwa na hoteli, nyumba za kulala wageni na baa Sh 130,000, biashara na viwanda, sekta ya kilimo na zingine ambazo hazijatajwa itakuwa Sh 100,000.
Kutokana na tofauti ya kima cha chini kulingana na sekta, Tucta iliomba mfumo wa kupanga mishahara, urudi kama zamani, ambapo kima cha chini kilikuwa cha aina moja.
Hata hivyo, alielezea kuridhika kidogo katika tangazo la mishahara ya kisekta, huku akisema bado kunahitajika nyongeza kutokana na hali halisi ya maisha ilivyo sasa kwani kila kitu kiko juu.

Comments

Popular Posts