Saturday, July 6, 2013

WARIOBA AWAONYA VIONGOZI WA SIASA, DINI KUHUSU RASIMU YA KATIBA...

Jaji Joseph Warioba.
Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba amevionya vyama vya siasa, watu na taasisi zikiwamo za kidini, kuacha kuingilia wajumbe wa mabaraza ya Tume ya Katiba wakati huu wanaojiandaa kutoa maoni katika mchakato wa maboresho ya Rasimu ya Katiba mpya.

Aidha, amesisitiza kuwa suala la serikali tatu ambalo mapendekezo yake yameguswa sana katika Rasimu hiyo na kusababisha mijadala katika maeneo mengi, lisingeweza kuepukika, kutokana na kuzungumzwa sana kwa kipindi cha miaka 30.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, alipozungumzia kuanza mikutano ya Mabaraza ya Katiba Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu katika wilaya zote nchini.
Alisema ili mchakato huo ufanyike kwa ufasaha na kupatikana kwa Katiba mpya, ni vema vyama vya siasa na taasisi hizo, vikawaacha wajumbe hao watoe maoni kwa maslahi ya Taifa na si kwa mtu au makundi.
Alisema mchakato wa kuanza kwa mabaraza hayo, umekuja wakati Tume tayari imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusambaza nakala za Rasimu nchini, ambako mabaraza hayo yatakuwa yakitoa maoni.
"Tunatarajia mabaraza yatatoa mapendekezo kwa kina na kwa uhuru, hii ni nafasi kwa wajumbe hao ambao tuna imani kuwa wamepata muda mzuri wa kuchambua Rasimu na kupata mawazo ya wananchi wengine ili kuwa tayari kwa majadiliano katika mabaraza ya wilaya," alisema Jaji Warioba.
Aidha, alisema jumla ya wajumbe 19,333 nchini wakiwamo 1,874 wa Tanzania Bara na 1,158 wa Zanzibar, walipewa nakala za Rasimu huku 40 zikipelekwa katika kila kijiji, mitaa na shehia ili kuwezesha wananchi kupata fursa za kuzisoma na kuchangia mawazo.
Juu ya utaratibu wa mabaraza hayo, alisema Tume imeweka ushiriki mpana kwa kila mjumbe kuchangia na kutoa mawazo kwa uhuru na uwazi, huku akisisitiza kuwa kinachopaswa kufanywa na wajumbe ni kutoa maoni na si malalamiko.
Alisema kwa upande wa mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana, watatakiwa kuandaa mikutano ya kutoa fursa kwa wanachama wao ili kutoa maoni juu ya rasimu hiyo na kuyawasilisha kwa Tume ifikapo Agosti 31.
Kuhusu suala la muundo wa serikali tatu, lililojitokeza katika Rasimu hiyo, Warioba alisema mbali na maoni ya wananchi wengi kuhusu suala hilo, maoni ya serikali moja na mbili pia yalijitokeza, isipokuwa la serikali tatu ndilo lilikuwa na umuhimu mkubwa, kwa kuwa limezungumzwa kwa muda mrefu.
ÒKwa zaidi ya miaka 30 sasa suala hili limekuwa likizungumzwa, kila upande unaona kuna mambo yanapaswa kufanyiwa marekebisho, wapo waliosema tuvunje Muungano na wengine kushauri ufanyiwe marekebisho, sasa yote kwa pamoja tuliona vema tulikabidhi kwa wananchi ili kuliamua wenyewe,Ó alisisitiza Jaji Warioba.
Alisema mapendekezo kuhusu suala hilo na mengine yatayopatikana, yatawezesha mchakato huo kusonga mbele kwa hatua ya Bunge la Katiba kabla ya hatua nyingine kufuata.

No comments: