![]() |
| Rais Barack Obama. |
Ili kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa umeme katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Marekani imeamua kuanzisha miradi kwa ajili hiyo.
Taarifa zilizopatikana kwenye msafara wa Rais Barack Obama anayezuru Afrika hivi sasa, zimesema kwa kuanzia, Taifa hilo litafanya kazi na Ethiopia, Ghana, Kenya, Liberia, Nigeria na Tanzania.
Wataalamu wanakubali kwamba ukosefu wa nishati ya umeme ni kikwazo kwa maendeleo ya Afrika. “Afrika kwa kiasi kikubwa ni bara la giza usiku,” alipata kusema ofisa wa shirika kubwa duniani ambaye hakutaka kutajwa jina. “Kwa kila jinsi unavyoliangalia suala hili, Afrika iko nyuma na inatumia gharama kubwa.”
Kwa makadirio ya haraka haraka, theluthi mbili ya Afrika Kusini mwa Sahara haina umeme, kiwango ambacho kwa vijijini ni kikubwa hadi asilimia 85, mfanyakazi wa Ikulu ya White House, Gayle Smith alisema.
Ukosefu wa umeme unazuia uwekezaji katika biashara, unazuia watoto kusoma usiku na kuwa kazi nzito kuhifadhi chanjo bila kuharibika hususan maeneo ya vijijini, alisema.
“Marekani itaanza kufanya kazi na Ethiopia, Ghana, Kenya, Liberia, Nigeria na Tanzania katika uzalishaji umeme, maofisa wa White House walisema na kuiongeza kuwa pia itashirikiana na Uganda na Msumbiji katika uzalishaji mafuta na gesi.
Mpango huo utahusisha mashirika mengi ya Serikali ya Marekani ili kufikia malengo. Mathalan, Shirika Binafsi la Uwekezaji Nchi za Nje la Marekani (OPIC) litatoa dola bilioni 1.5 pamoja na bima kusaidia kampuni za kimarekani kukabiliana na hatari zinazoweza kutokea wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Hali kadhalika benki ya Export-Import pia ya Marekani itatoa dola bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia kuendeleza miradi hiyo bya umeme, maiofisa hao waliongeza.
Sekta binafsi nayo itahusishwa. Maofisa hao walisema kampuni ya General Electric imesaini makubaliano ya kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme Tanzania na Ghana, maofisa hao waliongeza.
Ingawa ugonjwa wa Mandela umegubika ziara ya Obama lakini kote alikopata fursa ya kuzungumza tangu akiwa Senegal na Afrika Kusini, alisisitiza fursa ya maendeleo iliyoko barani Afrika.
Katika kusisitiza hilo, Obama anatarajiwa kutangaza pia kuwa ana mpango wa kuitisha mkutano wa wakuu wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara utakaofanyika jijini Washington, Marekani mwakani.
“Ni kitu ambacho nchi zingine zimeshafanya,” Rhodes alisema. “Tunachotaka kufanya ni kuendelea na haya tuliyokwishayazungumza na viongozi katika ziara hii.”
Marekani haijihisi kutishwa na kukua kwa biashara na uwekezaji wa China katika Afrika na mataifa mengine makubwa yanayochipukia, Obama alisema juzi.
Mawazo kuwa ameruhusu China kuipiku Marekani katika kufanya biashara na Afrika yalitawala ziara hiyo, lakini alisema kuingezeka kwa biashara ya China katika Afrika kuna manufaa kwa wote.
“Sihisi kutoshwa na hilo. Nadhani ni kitu kizuri tu,” Obama aliwaambia waandishi wa habari. Nchi zinavyozidi kuwekeza Afrika, bara hili ambalo liko chini kijaendeleo duniani litaweza kuingia katika uchumi wa dunia, alisema.
China imejitanua katika Afrika tangu kuanza kwa karne mpya. Iliipita Marekani kama mbia mkubwa wa biashara na kwa Afrika mwaka 2009, ripoti ya Februari iliyotolewa na Ofisi ya Uwajibikaji ya Serikali ya Marekani (GAO) inaonesha.
Manufaa inayopata China katika biashara yanatokana na kiasi cha bidhaa inazouza Afrika. Mauzo ya China kwa Afrika mwaka 2011 yalizidi ya Marekani mara tatu.
Inapokuja katika uwekezaji, hata hivyo, picha inakuwa tofauti. Takwimu za kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 zinaonesha, kwamba uwekezaji wa Marekani katika Afrika ulikuwa mkubwa kuliko wa China, kwa mujibu wa GAO.
“Nafasi ya China kama mwekezaji, mhisani na mfadhili ni kubwa sana,” Deborah Brautigam ambaye alisoma China na sasa yuko katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins aliandika hivi karibuni.
“Ingawa nchi za Magharibi zina wasiwasi na kukua kwa nafasi ya China katika Afrika, Marekani peke yake ilitoa fedha nyingi kwa nchi za Afrika kuliko China ilivyofanya mwaka 2010,” aliandika.
Bado, nafasi ya China ni kubwa barani humo, kwa sababu imefanya bidii kubwa katika uwekezaji wake. China na Marekani zinapaswa sasa kuwa wabia Afrika, ili kudumisha maendeleo na amani, ilisema taarifa ya China baada ya kauli ya Obama.
Ziara ya Obama Afriak Kusini na Tanzania inatoa taswira ya ziara ya Machi ya Rais wa China Xi Jinping, ambao ingeweza kuonesha uadui baina ya mataifa hayo mawili makubwa katika Afrika, shirika la habari la China Xinhua lilisema.
“Hizi ni fikra za kizamani. Zinatokana na jinsi Magharibi ilivyokuwa inaichukulia dhima ya China katika Afrika ,” Xinhua ilisema. “Pia inakosa picha halisi ya China na Marekani, ambayo badala ya kuwa washindani na kudharauliana, zinaweza sasa kufanya kazi kama wabia katika kuleta maendeleo ya Afrika”.
Akizungumza Pretoria juzi, Obama alizitaka nchi za Afrika kuwa na msimamo imara kwenye majadiliano ya uwekezaji kutoka nje.
“Mnazalisha malighafi, mnaziuza rahisi na mwishowe kuna mtu mwingine anatengeneza fedha na ajira lakini pia na thamani yake,” alisema.
“Hakikisheni yeyote mnayejadiliana naye … muingie katika makubaliano mazuri ambayo yatanufaisha watu wenu na yanayoweza kusaidia kuleta maendeleo,” alishauri.
Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), imelenga kutoa dola bilioni 1.63 kusaidia miundombinu ya nishati ya umeme kwa nchi sita za Afrika ikiwamo Tanzania.
Taarifa kutoka AfDB zimesema, fedha hizo zinahusu nchi sita zilizo kwenye mpango wa miaka mitano iliyopita, ikiwa ni pamoja na dola bilioni 1.4 chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Afrika (ADF) kwa ajili ya mikopo ya bei nafuu kwa nchi za kipato cha chini. Marekani ni mchangiaji mkubwa wa ADF yenye miaka 13 tangu ianze.
Rais wa AfDB, Donald Kaberuka alitarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya ziara ya Rais Obama, katika mpango unaolenga juhudi za kuchangia kukuza uchumi na maendeleo ya Afrika kupitia ongezeko la upatikanaji umeme wa uhakika na wa bei nafuu.
Mpango huo ni wa ushirikiano wa wadau ikiwamo Marekani, Benki hiyo na nchi sita za Afrika. Ambao unalenga kuongeza upatikanaji umeme wa uhakika, kuongeza biashara ya nishati hiyo mipakani na kukuza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za nishati.
Aidha, Dk Kaberuka atazungumzia mpango wa AfDB kusaidia kuboresha utawala bora katika Kituo cha Sheria cha Afrika, ambacho husaidia nchi wanachama wa kikanda kujadili mikataba ya rasilimali za madini, kuwezesha mazingira na mifumo ya kisasa ya kisheria na udhibiti.

No comments:
Post a Comment