![]() |
| Stendi Kuu ya Mabasi ya Mikoani, Ubungo, Dar es Salaam. |
Abiria wa mabasi yaendayo Arusha, Moshi, Morogoro na Dodoma, wamejikuta katika wakati mgumu katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, Dar es Salaam.
Hali hiyo ilitokana na kupandishwa ghafla kwa nauli, baada ya kuongezeka kwa mahitaji wa huduma hiyo, kwa kuwa shule nyingi za sekondari zimefunguliwa.
Mwandishi jana alishuhudia msongamano wa watu katika kituo hicho kuanzia saa mbili asubuhi, huku kukiwa na idadi ndogo ya mabasi yaendayo mikoa ya Kaskazini, tofauti na ilivyozoeleka.
Mwandishi alishuhudia hakuna basi lililokuwa likitangaza safari ya Arusha kwa abiria waliokuwa wakikata tiketi nje ya ofisi na wala hapakuwa na kondakta au mpigadebe aliyehangaika kung'ang'ania abiria kama ilivyo kawaida.
Kilichokuwa dhahiri ni abiria kuomba nafasi ya kusafiri kana kwamba wanasaidiwa huku wahusika wakisisitiza kuishia Moshi.
Uchunguzi wa gazeti ulibaini kuwa ofisi za kukatisha tiketi kwa mabasi ya Arusha, Moshi, Dodoma na Morogoro, ndizo zilizokuwa na matatizo zaidi kwa sababu ziliamua bila utaratibu kutoza nauli ya kati ya Sh 22,000 na Sh 40,000 na kusababisha abiria wengi washindwe kusafiri.
Vile vile, ilithibitishiwa na abiria kituoni hapo kuanzia saa 11 alfajiri jana, kwamba mabasi mengi yaliyokuwa yanapaswa kuanza safari saa 12 asubuhi yaliondoka kabla ya muda, kwa kuwa yalijaa haraka baada ya abiria kuridhia kulipa Sh 40,000 kwa yaendayo Moshi na Arusha.
Shafuri Mgonja alikuwa kituoni hapo tangu saa 11 alfajiri, lakini alishindwa kusafiri kwa maelezo kuwa mabasi yaliyokuwapo yalikataa abiria wa Arusha na kusisitiza kuishia Moshi kwa nauli ya Sh 40,000.
"Wamenivurugia ratiba kwa sababu usafiri wa kwenda huko unajulikana nauli yake ni Sh 32,000, hebu fikiria umejipanga kusafiri kwa kiasi hicho halafu unafika hapa unaambiwa na wahusika kuwa nauli ni Sh 40,000, na hata hivyo, hiyo inakufikisha robo tatu ya safari na si mwisho wa safari, utasafiri kweli," alilalamika na kuhoji huku akiwa na hasira ya kutibuliwa ratiba zake.
Maimuna Mketema aliyekuwa aende Arusha naye alidai alipaswa kusafiri na mdogo wake kwenda shuleni lakini walikwama kutokana na kupandishiwa nauli bila taarifa.
Kwa maelezo yake, walikuwa kituoni tangu saa 12 asubuhi lakini hawakupewa tiketi katika gari la Osaka walilokuwa wakilitaka kwa sababu hawakuwa na Sh 40,000.
"Inasikitisha kwa kweli kwa sababu mdogo wangu anakwenda shule, anasoma Moshi na nauli tuliyokuwa nayo ni Sh 28,000 kwa kila mmoja, wao wametaka Sh 40,000 kana kwamba wanatupeleka Arusha sasa imebidi tubaki kusubiri majaliwa kama itatokea bahati tuondoke hata kwa kupanda Coaster, vinginevyo tunarudi nyumbani," Mketema alisema.
Kwa upande wa abiria wa Dodoma na Kilombero, hali ilikuwa ngumu pia, ambapo mabasi yaliyokuwepo yaliendesha mgomo baridi wa kutokuondoka na abiria waliolipa nauli chini ya Sh 22,000 wakati nauli halali ya kwenda Dodoma ni Sh 17,000.
Basi la Saibaba liendalo Rombo mkoani Kilimanjaro nalo liliondoka kituoni kabla ya muda huku likiwa limewatoza abiria Sh 27,000 badala ya Sh 22,000 iliyopangwa na Serikali. Hata hivyo, namba za usajili wa basi hilo hazikuweza kupatikana kwa sababu wahusika hawakuziandika katika tiketi kama inavyostahili.
Wakati hayo yakiendelea, timu ya maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Leo Ngowi ilifika kituoni hapo na kukamata magari hayo na kuamuru yarejeshe nauli za ziada yaliyotoza.
Kwa ushirikiano na polisi waliokuwa kituoni hapo, maofisa hao waliwezesha kukamatwa kwa wapiga debe wawili waliokuwa wakichochea kutozwa kwa nauli za juu na 'kuwahifadhi' katika rumande ya kituo kidogo cha Polisi ndani ya stendi hiyo.
Katika kamata hiyo iliyohusisha ukaguzi wa tiketi na kusikiliza abiria waliokuwa wakilalamika ndani na nje ya mabasi, iligundulika pia kuwa baadhi ya wahusika wa mabasi hawaandiki nauli wanayotoza katika tiketi wala namba za usajili wa mabasi yao ili kupoteza ushahidi wanapokamatwa kwa kukiuka sheria za usafirishaji huo.
Ngowi aliyezungumza na gazeti hili kituoni hapo alisema ni kweli wahusika wa mabasi yaendayo njia hizo wamekiuka taratibu na sheria ya usafirishaji kwa kutoza nauli kubwa bila kuwa na sababu za msingi.
"Kwa bahati mbaya tulichelewa kugundua tatizo hili leo (jana) ndio maana mabasi mengine yaliwahi kutukimbia asubuhi kabla ya muda wao wa kuondoka. Lakini tunashukuru, kwamba tulipata taarifa na kuja wenyewe kujionea hali halisi. Tumechukua hatua hadi sasa na kuyaorodhesha magari yaliyozidisha nauli kwa ajili ya hatua za kisheria," alisema.
Sambamba na kuyaorodhesha, mwandishi alishuhudia makondakta wa mabasi yaendayo Arusha, mfano Happy Nation namba T 892 BBA waliotoza Sh 40,000 badala ya Sh 32,000 kwa safari ya Arusha wakiamriwa warejeshe nauli ya ziada, na baada ya kutimiza agizo hilo, liliruhusiwa kuendelea na safari.
Lakini, Ngowi alikuwa na orodha ndefu ya mabasi waliyoamuru yarejeshe nauli kuwa ni pamoja na Osaka namba T 201 CJZ liendalo Arusha ambalo wahudumu wake walitoza Sh 40,000, Happy Nation namba T 939 BMK iendayo Arusha pia ikitoza Sh 40,000, New Central namba T 286 AAF liendalo Dodoma lililotoza Sh 22,000 badala ya Sh 17,000 na basi lingine la Dodoma, Al-Saedy namba T513BEF lililotoza Sh 22,000 isivyo halali.
"Katika hayo yaendayo Dodoma, basi la Al-Saedy lilitutoroka hapa kituoni bila kurejesha kwa abiria nauli ya ziada iliyotozwa. Hilo ni kosa litakalotufanya tulifungie kwa sababu tulizungumza nao wakakiri kosa na kukubali kurudisha nauli kabla ya kuendelea na safari sasa wamekimbia.
"Tulichofanya, tumepiga simu kwa maofisa wetu na askari wa usalama barabarani ili wakamatwe Morogoro. Saibaba ya Morogoro nayo kweli ilifanya ukaidi na kuondoka kabla ya muda huku ikiwa imetoza nauli zaidi ya ile ya halali. Tunaifuatilia kwa sababu ilishaondoka na kuhusu namba pia bado tunazitafuta kujua ni lipi".
Kwa maelezo ya Ngowi, mabasi yapo ya kutosha isipokuwa wahusika huamua kuyaondoa mapema au kuyafungia kwa sababu ya kutaka kupandisha nauli bila utaratibu.
"Kwa sababu hiyo wanasababisha uhaba kwa makusudi na kufanya watu wafikirie kwamba pengine tumeyafungia. Hata hivyo, kutokana na hali ya leo (jana), uhaba huu hausababishwi na SUMATRA hatujafungia mabasi ya njia hizo na hata tukiyafungia inakuwa ni baada ya ukaguzi na kujiridhisha kuwa ni lazima yaondoke barabarani," Ngowi alisema.
Kutokana na hali hiyo, Ngowi aliomba abiria wasiwe wepesi kukubali kuchuuzwa kwa sababu ni kuvunja sheria na miongozo ya usafiri wa nchi kavu, badala yake, watoe taarifa kwa mamlaka ili ziingilie kwa haraka na kutatua matatizo kama ilivyofanya jana.
"Ni mwito na onyo pia kwa wasafirishaji wa mabasi kwamba tutakuwa Ubungo kuhakikisha mchezo huo haujirudii. Wananchi tupeni taarifa za wanaovuruga ratiba na gharama za usafiri ili wachukuliwe hatua," alisema.

No comments:
Post a Comment