Saturday, July 6, 2013

MTUHUMIWA WA UGAIDI UINGEREZA AKAMATWA TANZANIA KWA WIZI WA PASIPOTI...

Robert Manumba.
Jeshi la Polisi nchini limesema raia wa Uingereza, anyetuhumiwa kwa ugaidi nchini mwake, yumo nchini akishitakiwa kwa tuhuma za wizi wa pasipoti za Tanzania.

Mwingereza huyo mwenye pasipoti mbili; ya Tanzania namba AB 651926 na nyingine ya Uingereza ambayo haikutajwa namba ni mmoja kati ya watuhumiwa wawili wa ugaidi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, pasipoti ya Tanzania ni miongoni mwa zilizoibwa Uhamiaji na Mtanzania  aliyedai kuwa ni mwanafunzi anayesoma Sudan.
Kutokana na maelezo ya Manumba, Mwingereza huyo anayeonekana kwa picha tofauti katika pasipoti hizo mbili, akiitwa Adil Ally Patel katika pasi ya Tanzania na  Iqbal Hassan Ally kwa ile ya  Uingereza, ni miongoni mwa watu wanaotafutwa na nchi hiyo ya Ulaya kwa tuhuma za ugaidi.
"Tumewasiliana na Uingereza wamekiri ni raia wao wanayemtafuta kwa tuhuma za ugaidi. Tulimkamata hivi karibuni katika mpaka wa Kasumulu akitoka nchini kwenda Malawi. Anajiita Mtanzania lakini hajui Kiswahili.
ÒBaada ya kushukiwa na kupekuliwa alikutwa na pasipoti hizo na kompyuta mpakato yenye maandishi mengi ya kichochezi dhidi ya dini asizoziabudu. Maneno katika kompyuta yake yanasisitiza kuteketezwa kwa watu wa dini nyingine (hakuzitaja)," alisema Manumba. Taarifa zaidi zilisema mtuhumiwa huyo, alifikishwa mahakamani jana (Soma zaidi Uk 32).
Kutokana na hali hiyo, Polisi imetoa hadhari kwa umma juu ya kuwepo kwa chembe za ugaidi nchini na kuwataka raia watoe taarifa pindi wagunduapo watu au vikundi visivyoeleweka, kwa sababu ndivyo vinavyotumika kuendesha ugaidi na kuvuruga usalama.
Aidha, Manumba alisema Polisi inachukulia kwa uzito wa juu taarifa zinazotolewa na wananchi, vikiwamo vyombo vya habari, kwa sababu licha ya kuwa na vyanzo vya kiintelijensia vinavyoshirikiana na vyombo vingine vya usalama duniani, taarifa za wananchi hao zimechangia usalama uliopo kwa kiasi kikubwa.
Manumba alisema matukio ya mabomu ya Arusha na Zanzibar ni ishara ya kuwapo watu au vikundi   vinavyochochea upotevu wa amani nchini, kwa kufadhili ugaidi, kuusimamia  na kuhakikisha unatekelezwa.
"Tuna taarifa nyingi za kiintelijensia zinazoonesha kuwa hali si salama sana kwa upande wa ugaidi. Kutokana na hilo, tunaomba Watanzania wawe makini na watu au vikundi vya watu vinavyoashiria kuwa na msimamo mkali wa kidini kwa sababu wengi wao wanajihusisha na ugaidi huku wakijificha katika mwavuli wa dini," Manumba alisema.
Mbali na hayo, alisema mtuhumiwa huyo ndiye aliyetaja Mtanzania anayeshikiliwa na Jeshi hilo pia kuwa ni mshirika wake, ingawa kijana huyo aliliambia  Jeshi la Polisi kwamba yeye ni mwanafunzi tu katika shule moja nchini Sudan.
"Anajitetea, lakini tuliyoyakuta kwenye kompyuta yake ni kama yaliyo pia kwenye kompyuta ya mwenzake Mwingereza. Ni maandishi ya uchochezi wa hatari dhidi ya dini wasizoabudu. Kuna mahubiri pia yenye kuonesha msimamo wao mkali wa kiimani dhidi ya waumini wa dini zingine," aliongeza Manumba.
"Bado tunawashikilia na tunaendelea kuwasiliana na Sudan kupata ukweli. Huyu wa Uingereza naye tunaendelea kumchunguza na kupata uhakika wa namna alivyopata pasipoti ya Tanzania kwa sababu ni moja ya 26 zilizotangazwa kuibwa kutoka Uhamiaji," alisema.
Kutokana na taarifa hizo za ugaidi, Manumba alitaka wazazi wawasiliane na Polisi mara watoto wao wanapowaeleza kwamba wamepata vyuo au shule nje ya nchi. Alisema, wengi wamekuwa wakidanganywa na kuishia kwenye taasisi au shule zinazofundisha  ugaidi.
 "Tulitaharuki na kujua ukweli huo baada ya tukio la kigaidi la mwaka 1998 nchini ulipolipuliwa ubalozi wa Marekani. Vijana wetu walihusishwa na tulikuja kugundua kuwa wamekuwa wakipewa mafunzo katika vyuo hivyo Pakistan na Afghanistan," alisema.
Aliongeza kuwa wazazi, walezi, ndugu na jamaa wasifurahie kuchaguliwa kwa watoto wao kwenda  kusoma nje hadi polisi watakapowahakikishia kuwa vyuo, taasisi na shule wanazokwenda kusoma hazipo katika orodha mbaya waliyonayo.
"Lindeni watoto wenu, watu wanaowashawishi kujiunga na ugaidi tunao humu humu nchini na wengi wao wanajificha katika mwavuli wa dini, polisi tuko makini kubaini lakini taarifa zenu na ushirikiano wenu utatusaidia kuwakomesha," alisema.
Kuhusu mabomu ya Arusha, alisema tayari wamepata taarifa za uhakika kutoka China kuwa bomu mojawapo lilitengenezwa nchini humo na kuuzia taasisi, ambayo hata hivyo wanafuatilia kujua ni ipi na lilitokaje huko na kuingia nchini.
"Hatuwezi kukubali watu wasio na hatia wapate ulemavu au kupoteza maisha, kana kwamba hakuna Jeshi wala Serikali, ndiyo maana tunafanya kazi kuhakikisha tunazuia uhalifu na kupata wahusika wa uhalifu.
"Tumejua sasa kuwa bomu lilitoka China kinachofuata ni kutuma maelezo yote muhimu ili watufahamishe mambo mengine ikiwamo taasisi iliyouziwa bomu hilo. Ukweli utawekwa wazi," alisema Manumba.
Bomu hilo lirushwa katika mkutano wa Chadema uliofanyika katika viwanja vya Soweto, Kaloleni, wakati chama hicho cha upinzani kikikamilisha kampeni zake za kuwania udiwani Juni 15 na kuua watu wanne na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Manumba alisema pia kuwa zipo taarifa za kuwapo kikundi cha kigaidi cha al Shabab, ambacho kimekuwa kikizunguka Afrika Mashariki, kutafuta mwanya wa udhaifu na kushambulia.
Katika hatua nyingine, Manumba alisema juzi Jeshi hilo lilikamata meno ya tembo 347 yakiwa yamefichwa katika nyumba Kimara, Dar es Salaam. 

No comments: