ASKARI SABA WA JWTZ WALIOUAWA DARFUR WALIPAMBANA KWA MASAA MAWILI...

Baadhi ya askari wa JWTZ wakipita mbele ya miili ya wenzao waliouawa mjini Darfur, kutoa heshima zao za mwisho kwenye viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi, Dar es Salaam jana.
Majeneza yenye miili ya askari hao yakiwa yamepangwa tayari kwa zoezi la kutoa heshima za mwisho.
Wanajeshi saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa wakati wakilinda amani  Darfur nchini Sudan, walipigana kwa saa mbili wakati wakijitetea kabla ya kufikwa na mauti.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akitoa salamu za rambirambi, wakati wa kuaga askari hao waliouawa Julai 13.
Katika shughuli hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa, Rais Jakaya Kikwete aliongoza waombolezaji kuaga mashujaa hao ambapo pia Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na mawaziri mbalimbali walihudhuria.
"Kikundi hicho (askari wa JWTZ) kilikuwa kikitokea eneo la Abeche, kwenda Nation na kilipofika umbali wa kilometa 25, doria hiyo ilipunguza mwendo kutokana na utelezi wa matope yaliyosababishwa na mvua.
"Ghafla kikundi hicho kilishambuliwa na watu ambao hawakufahamika, wakitumia silaha nzito za kivita," alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema ulikuwa ni mtego wa mashambulizi na kwa mujibu wa taratibu za operesheni hizo, doria hiyo haikuwa na silaha nzito, lakini ililazimika kujibu mapigano hayo hadi kikundi kingine cha askari wa JWTZ, kilipoitwa kuongeza nguvu kunasua wenzao katika mtego huo.
Jenerali Mwamunyange alisema wakati kikundi hicho kikinasuliwa, askari hao walipoteza maisha kwa ujasiri mkubwa na wengine 14 kujeruhiwa.
Alisema Tanzania imefikwa na msiba huo wa mashujaa, ikiwa imeshiriki  kulinda  amani  Sudan tangu mwaka 2007, ambapo askari wake wamekuwa wakitekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu, kwa kushirikiana na vikundi vingine na wenyeji katika maeneo ya operesheni.
Awali Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja,  alitaja majina ya mashujaa hao na mahali wanapokwenda kuzikwa, kuwa ni pamoja na  Sajini Shaibu Othman (Zanzibar) na Koplo Osward Chaulo (Kilolo, Iringa).
Wengine ni Koplo Mohammed Ally (Zanzibar), Koplo Mohammed Chukulizo (Kigoma), Praiveti Rodney Ndunguru (Songea), Praiveti Fortunatus Msofe (Tanga) na Praiveti Peter Werema (Tarime, Mara).
Akitoa salamu za rambirambi, Rais Kikwete alisema mauaji ya wanajeshi hao, yalimshitua, kumhuzunisha na  kumkasirisha na kujikuta akijihoji kwa nini watu wa Sudan waue Watanzania.
Alisema Watanzania hao walikwenda kuwasaidia kupata amani, utulivu, kunusuru maisha yao na kuwaondolea mazingira ya wasiwasi ili wafanye shughuli zao kwa tija.
Alisema tangu kuanza kwa shughuli za ulinzi wa amani Darfur, walinzi wa amani 41 kutoka mataifa mbalimbali wameuawa, na 55 kujeruhiwa na  hakusita kuamini kuwa waliofanya tukio hilo  ni wasiotaka amani Darfur.
"Idadi hii ni kubwa, inahitaji kutafakari vizuri na kutazama upya mfumo wa kiwango cha kujilinda kwa wanajeshi lazima uwezo huo uongezwe ili kupunguza vifo zaidi," alisema Rais Kikwete.
Aliahidi kufikisha maombi hayo kwa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN), ili walitazame vizuri.

No comments: