![]() |
| Winnie Mandela akizungumza na vyombo vya habari. |
Nelson Mandela anaonesha 'maendeleo makubwa' katika afya yake tangu siku chache zilizopita, mkewe wa zamani alisema jana.
Winnie Madikizela-Mandela alihabarisha kuhusu Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini wakati akiongea na vyombo vya habari nje ya nyumbani kwa zamani kwa Mandela mjini Soweto.
"Mimi si daktari, lakini ninaweza kusema kwamba kutoka vile alivyokuwa siku chache zilizopita kuna maendeleo makubwa, lakini kitabibu bado hayuko vizuri," alisema Winnie, ambaye pia ni mbunge katika Bunge la Afrika Kusini.
Wanafamilia ya Mandela na mawaziri wa Afrika Kusini wametembelea hospitali hiyo ambako Mzee Mandela mwenye miaka 94 yuko katika hali mbaya.
Imekuja baada ya binti yake, Makaziwe kusema juzi kwamba Mandela alikuwa akipata hisia anapoguswa na kujaribu kufungua macho yake, akiongeza: "Bado yupo."
Makaziwe alisema kwamba alipokwenda kumwona hospitalini alikuwa mwenye hisia na fahamu.
"Siwezi kuongopa, haionekani vizuri," alilieleza shirika la habari Afrika Kusini (SABC).
"Lakini tunapomuongelesha, anageuka na kujaribu kufungua macho yake. Bado yupo. Anaweza kuwa katika hali mbaya, lakini bado yupo."
Mzee Mandela amelazwa hospitalini hapo kwa matibabu ya maambukizi kwenye mapafu tangu Juni 8, mwaka huu.
Mandela, ambaye alikuja kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini baada ya kukomeshwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, alilazwa baada ya kupata maambukizi kwenye mapafu. Hii ni mara yake ya nne kulazwa tangu Desemba, mwaka jana.
Mzee Mandela alifungwa jela kwa miaka 27 chini ya utawala dhalimu wa makaburu na aliachiwa huru miaka 23 iliyopita, mwaka 1990. Kisha akashiriki kuunganisha taifa hilo lililogawanyika kutoka kwenye ubaguzi wa rangi na kuwa taifa linalofuata demokrasia sawa kwa wote.
Kama matokeo ya kujitoa mhanga kwake na juhudi zake za kuleta amani, anaonekana na wengi duniani kama alama ya mapatano.

No comments:
Post a Comment