Mwenyekiti wa kitongoji cha mjini Bunda anadai kuishi kwa hofu baada ya kutishiwa maisha na askari wa Polisi, akimtuhumu kufuatafuata wahalifu.
Akizungumza jana kwenye matembezi maalumu ya kuhamasisha ulinzi shirikishi, Ernest Nkonoki wa Mbulumatare, alidai kuwa kutokana na mazingira hayo, ari ya kushiriki ulinzi huo imepungua maana inaonekana kana kwamba maaskari wa Jeshi hilo wanashirikiana na wahalifu.
Akifafanua, Nkonoki alidai kuwa mazingira hayo yalianza siku aliyokamata vijana watano na kuwafikisha kituo cha Polisi cha hapa, wakidaiwa kuhusika na wizi majumbani kwa kukata nyavu za madirisha na kuiba baada ya kukiri na kuahidi kutoendelea na vitendo hivyo na hivyo kuachwa huru.
Hata hivyo, alidai kuwa siku chache baadaye, askari huyo (jina linahifadhiwa), alimfuata kumtaka aache umbeya na kufuatilia maisha ya watu hasa vijana “wanaotafuta maisha” huku akitishia kumkata kichwa akiendelea kufanya hivyo.
Nkonoki alidai kuwa ingawa alitoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo hicho cha Polisi, askari huyo alionywa baada ya kuomba radhi na kumhakikishia Mwenyekiti usalama wake, bado askari huyo anaendelea kumtamkia maneno hayo kila wanapokutana, hali inayomfanya akose amani.
Mkuu wa Kituo hicho cha Polisi, Raphael Mayunga licha ya kumhakikishia usalama Mwenyekiti huyo kwa mara nyingine, pia alimwomba asipoteze muda kuhangaika na askari huyo kwani ana matatizo ya akili, kauli iliyozua mjadala miongoni mwa wananchi wakitaka askari huyo kuachishwa kazi kama ana matatizo na afya ya akili yake.
Nkonoki aliifananisha hali hiyo na tukio la takribani miaka 13 iliyopita ambapo askari wa kituo hicho alijiua kama hatua ya kupoza hasira baada ya kushindwa kumwua mwenzake aliyekuwa akimtishia maisha baada ya kumtuhumu kufanya mapenzi na mke wake.
Alisema hali hiyo inamtia mashaka na hofu kwamba inawezekana hata askari huyo akaamua kumfanyia hivyo na kuhatarisha maisha yake.
No comments:
Post a Comment