| Mizengo Pinda. |
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana alihitimisha mjadala wa Bunge la 10 lililojadili na kupitisha Bajeti ya Serikali na bajeti za wizara mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa kila mbunge kuwajibika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu.
Akihutubia Bunge jana kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano huo, Pinda aliwataka Watanzania na viongozi nchini, wasijaribu kuweka nchi rehani kwa kuhamasisha kwa njia moja au nyingine kuvurugwa kwa amani.
Alikumbusha kuwa matukio ya vurugu ya hivi karibuni, mengi yanahusishwa na vyama vya siasa na kuongeza kuwa, wakati hayo yakitokea, wakumbuke sheria inakataza vyama vya siasa kujihusisha na vurugu, kuigawa nchi kwa udini, ukabila, rangi au aina yoyote ya ubaguzi, itakayosababisha kutoweka kwa amani.
“Vile vile Sheria imeweka bayana kuwa, chama kitakachobainika kufanya hayo, kitafutwa kwa mujibu wa sheria. Napenda kuwakumbusha viongozi wenzangu hasa wa kisiasa kwamba, demokrasia si kufuta vyama wala kuvuruga nchi na kuwagawa Watanzania, bali ni sera nzuri, zinazowaunganisha Watanzania na kudumisha amani,” alisema.
Pinda alisema ziko dalili za kuweko kwa vikundi vya watu wachache wasiotakia mema nchi, vinavyotaka kupandikiza chuki za kisiasa na kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta mapigano na mauaji miongoni mwao.
Alikumbusha baadhi ya vurugu zilizotokea katika kipindi cha mwaka mmoja tu, kuwa ni pamoja na katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Singida na Iringa. Alitaja pia hofu ya kidini iliyotokea Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Geita.
“Baadhi ya matukio haya, yamesababisha vifo na majeruhi ikiwemo kujeruhiwa kwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), uharibifu wa miundombinu, mazingira na mali za Serikali na watu binafsi,” alisema.
Alisema matukio hayo pamoja na lile la kulipua bomu kanisani na hivi karibuni katika mkutano wa hadhara wa Chadema katika Uwanja wa Soweto Arusha, yamesababisha hofu kubwa kwa wananchi na hisia ya kuwepo kwa tishio la kuendelea kwa vitendo vinavyoashiria ugaidi katika nchi.
“Sina shaka kuwa fujo, vurugu, vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwemo mashambulio ya mabomu Arusha na vurugu za Mtwara, ni sehemu ya mikakati hiyo mibovu (ya kikundi hicho),” alisema.
Akielezea hatua zitakazochukuliwa, Pinda aliwahakikishia Watanzania kwamba Serikali haitavumilia hata kidogo kuendelea kupandwa mbegu ya chuki za kidini na kisiasa miongoni mwa Watanzania.
“Serikali itachukua hatua kali bila huruma kumaliza njama hizi mbaya dhidi ya Taifa letu. Vile vile hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika, bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii,” alionya.
Aliwasisitizia viongozi wa Serikali, siasa, dini na wananchi, kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
“Tuendeleze mshikamano na kukataa vitendo vya uvunjifu wa amani kwa nchi yetu. Kila mwenye taarifa ya kuwezesha kukamatwa kwa watu wanaohatarisha amani ya nchi yetu, atoe taarifa kwa Jeshi letu la Polisi, na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na kwa maslahi ya Taifa,” alisema.
Pinda alisema Tanzania bado ni nchi nzuri na ina amani na Watanzania bado ni watu wazuri, wastaarabu, wavumilivu na wapenda amani.
“Wananchi wanaelewa na ni watiifu, twendeni tukasisitize umuhimu wa amani, upendo na mshikamano. Tukiwasimamia vizuri na kuwaongoza katika matumizi ya rasilimali zilizopo, nchi yetu itasonga mbele kimaendeleo na maisa bora kwa wananchi wetu, yatapatikana,” Pinda aliwaambia wabunge.
No comments:
Post a Comment