![]() |
| Rais Barack Obama akishuka kwenye ndege mara baada ya kuwasili nchini Afrika Kusini jana jioni. |
Rais Barack Obama amewasili Afrika Kusini jana jioni, lakini sasa hatamtembelea kinara wa kupinga ubaguzi wa rangi, Mzee Nelson Mandela hospitalini alikolazwa mjini Pretoria katika kituo chake cha pili cha ziara yake ya nchi tatu za Afrika.
Rais huyo wa Marekani hakuwa na mpango wa kukutana na wananchi hiyo jana na kulikuwa na matumaini kwamba angeweza kufunga safari kwenda hospitalini baada ya hapo.
Hatahivyo ripoti kutoka Afrika Kusini zinasema familia ya Mandela ilikuwa ikiondoka hospitalini usiku huo na hakukukuwa na wageni wengine zaidi jioni hiyo.
Hali ya baba huyo wa taifa bado inaelezewa kuwa mbaya lakini inaimarika, ingawa hali yake kwa ujumla inafahamika kwamba imezorota.
Akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi kabla ya kupanda ndege yake ya Air Force One wakati wa safari yake kutoka Senegal kwenda Johannesburg, Obama alisema: "Tutaona hali ilivyo tutakapofika."
"Nafikiri meseji muhimu tutakayotaka kufikisha, kama si moja kwa moja kwake, lakini kwa familia yake, ni shukrani za kina katika uongozi wake," alisema Obama.
Ziara ya Obama ya siku tatu inahusisha ziara ya Kisiwa cha Robben mjini Cape Town, ambako Mandela alitumikia miaka 18 ya kifungo chake cha miaka 27 chini ya serikali ya makaburu wa Afrika Kusini.
Ikulu ilisema ilikuwa ni juu ya familia hiyo kuamua kama Obama anaweza kumtembelea hospitalini rais huyo wa zamani anayeumwa.
Mandela, mwenye miaka 94, anapambana na maambukizi kwenye mapafu ambayo yamemfanya awe kwenye hali mbaya na kulazwa hospitalini kwa karibu wiki tatu sasa ambapo imeelezwa anapumua kwa mashine..
Wakati huohuo, binti mkubwa wa Rais mstaafu Nelson Mandela aitwaye Makaziwe, amesema baba yake anasikia na anajaribu kufumbua macho akisemeshwa.
Makaziwe amesema hayo huku akiponda vyombo vya habari vya kimataifa na kuvifananisha na tai kutokana na habari vinavyotoa kuhusu afya ya kiongozi huyo.
“Hali yake si nzuri, lakini ukimsemesha anajitikisa na kufumbua macho kidogo,” alisema Makaziwe Jumatano usiku alipoombwa kuzungumzia hali aliyonayo baba yake baada ya kumwona wodini alimolazwa.
Wanaomtakia afueni wameendelea kujikusanya nje ya Hospitali ya Medi-Clinic jijini hapa wakiimba na kuomba kama ilivyo pia nyumbani kwake maeneo ya Soweto.
Watu wana hamu ya kujua maendeleo ya afya yake huku pia wakitaka kuonesha jinsi wanavyojivunia kiongozi huyu ambaye wanamwona kama Baba wa Taifa.
Limekuwapo ongezeko la ujumbe wa kumtakia afueni huku pia matangazo ya shukrani yakibandikwa katika kuta za hospitali hiyo.
Mabango mengi yaliyobandikwa yana picha za sura ya Mandela ambaye kiukoo anajulikana kama Madiba.
Watoto wamerusha angani maputo 94-moja kwa kila mwaka kuashiria umri wake ikiwa ni heshima kwake.
“Hakuna masikitiko hapa. Kuna sherehe. Ni shujaa,” Nomhlahla Donry (57), ambaye mumewe alitumikia Serikali na Mandela, aliiambia AFP.
“Tunasema aishi maisha marefu kwa sababu tunampenda amefanya mengi kwa ajili yetu katika dunia hii. Amefanya mambo mengi ya kuvutia na hakika tunampenda tata (baba),” mkazi wa hapa Alfred Makhatini aliiambia Reuters.

No comments:
Post a Comment