![]() |
| Dk Shukuru Kawambwa. |
Wakati Bunge likiendelea na vikao huku zikiwa zimebaki wizara tatu ambazo bajeti zake hazijasomwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatarajiwa kuamsha mjadala mkali bajeti yake itakaposomwa leo.
Ingawa wizara nyingine, ikiwemo ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia iliyosomwa jana, pia zitakuwa na hoja mbalimbali zitakazoibuliwa na wabunge, kwa upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012 na hatua ya Serikali kuyapanga upya, yataibua upya mjadala miongoni mwa wabunge.
Matokeo hayo yalitangazwa kwa mara ya kwanza Februari 18, mwaka huu. Kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kufeli, Serikali iliyafuta na kuamuru Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kufanya uchakataji upya kabla ya mapya kutolewa wiki iliyopita.
Katika matokeo mapya yaliyotangazwa, watahiniwa waliopata daraja la sifuri wamepungua kutoka 240,903 katika matokeo ya awali hadi kufikia 210,886.
Mbali na kupungua kwa idadi ya wanafunzi waliofeli, matokeo hayo mapya yanaonesha kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kidato hicho ukilinganishwa na matokeo ya awali, umepanda kutoka asilimia 34.5 hadi kufikia asilimia 43.08.
Mambo mengine ambayo yamekuwa yakijadiliwa kwa kina katika bajeti ya wizara hiyo, ni pamoja na ukosefu wa walimu wa kutosha, madarasa, maabara hususan katika shule za sekondari za kata.
Licha ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo bajeti yake itajadiliwa kwa siku mbili, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia iliyosomwa jana na kujadiliwa kwa siku moja, pamoja na masuala mengine, mjadala ulikuwa pia upande wa kampuni za simu za mkononi.

No comments:
Post a Comment