Sunday, May 12, 2013

MFANYABIASHARA ANAYELAWITI WANAFUNZI MWANANYAMALA ATIWA MBARONI...

Kamanda Charles Kenyela.
Jeshi la  Polisi  Mkoa wa Kinondoni  linamshikilia  Ahmad  Mohamed  Sharif (38), mfanyabiashara na mkazi wa Mwananyamala Msisiri ’A’ kwa tuhuma za kuwaingilia kinyume cha maumbile wanafunzi wanne wa darasa la nne wa Shule ya Msingi Misisiri ’A’.

Ahmad amekuwa akiwaingilia kinyume cha maumbile wanafunzi hao katika kipindi cha mwezi Aprili na Mei mwaka huu kwa nyakati tofauti. Kati ya wanafunzi  hao,  wawili wana umri wa miaka 10 na wengine wawili wana umri wa miaka 12 na 11 wote wakiwa ni wanafunzi wa Misisiri A.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Suzana  Orege (35)  alisema wanafunzi  hao  wamekuwa na mahudhurio mabaya shuleni kwa zaidi ya mwezi mmoja na ndipo walipojaribu kuwafuatilia kwa karibu ili kubaini  sababu za wanafunzi hao kutohudhuria shuleni.
Suzan  alisema ilipofika  Mei 9, mwaka huu walifanikiwa  kuwapata wanafunzi watatu (majina yanahifadhiwa) lakini mmoja alikimbia kusikojulikana  na walipowahoji sababu za wao  kutohudhuria  masomo,  waliwaeleza  kuwa huwa wanatoka nyumbani kama kawaida kwa ajili ya kwenda shule, lakini huishia nyumbani kwa Ahmed.
Alisema walipohojiwa zaidi walisema baada ya kufika nyumbani kwake huwawekea CD za  ngono  na kisha kuwaingilia kinyume cha maumbile  na kuwapa  maandazi, chapati, bagia, biskuti na kuwatishia wasiseme kwa  mtu yeyote na endapo watasema atawafanyia  kitu kibaya sana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishina  Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kenyela amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, ambapo alisema alikamatwa Mei 10, mwaka huu na  atafikishwa mahakamani kesho.
Kamanda  ametoa onyo kwa watu wengine wenye tabia chafu kama hiyo kuacha mara moja kabla ya kukumbwa na mkono wa sheria.

No comments: