![]() |
| Deus Kibamba. |
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, amekiri kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, haijawahi kutokea katika michakato ya nyuma ya marekebisho ya Katiba yaliyowahi kufanyika nchini.
Kibamba alitoa kauli hiyo jana huku akimwaga sifa kwa wajumbe wa Tume hiyo, kwamba ni wenye weledi, taaluma na uelewa wa hali ya juu, katika masuala mbalimbali ikilinganishwa na vipindi vya nyuma.
Akitoa mada kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, kwa wakurugenzi wa majimbo 34 ya Kanisa Katoliki nchini, katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Dar es Salaam, Kibamba alisifu pia mchakato uliotumika kuwapata wajumbe hao na utendaji kazi, kwamba ni wa kidemokrasia.
“Siku za nyuma wakati Katiba ikirekebishwa, Rais aliamka Ikulu na kutangaza wajumbe wa Bunge la Katiba, sasa hivi hata Rais alipoteua Tume, Sheria ilimtaka awasiliane na maeneo ama vikundi watu wanakotoka.
“Alindika barua kuomba apendekezewe majina matatu, ili achaguliwe mmoja ama wawili kati ya hayo majina,” alifafanua Kibamba.
Kwa mujibu wa Kibamba, hatua hiyo ya Rais Kikwete, inadhihirisha kuwa ipo demokrasia, hasa kutokana na aina ya wajumbe waliounda Tume, kuwa na weledi, taaluma na uelewa mkubwa, ikilinganishwa na vipindi vilivyopita vya marekebisho ya Katiba vilivyoundiwa.
Akiwataja kwa majina, Kibamba alisema Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba, Profesa Mwesiga Baregu na wengine wengi, ni magwiji katika masuala mbalimbali yanayogusa siasa na jamii.
Hata hivyo, Kibamba alisema ugwiji pekee hautoshi kufanya Katiba mpya ipatikane.
“Ugwiji pekee si sifa ya kufanya Katiba mpya ipatikane, matamko yanayotolewa na asasi, taasisi za kidini na watu binafsi hivi leo, ningekuwa mimi Warioba, nisingebeza wala kupuuza bali kuchambua hoja na kufanyia kazi,” alisema.
Juzi, Jaji Warioba alisema hazuii Jukwaa hilo kwenda mahakamani kuishitaki Tume, na kwamba hata katika uundwaji wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba, zipo asasi zimeomba kuunda mabaraza hayo, hivyo haelewi Jukwaa sasa ni nani.
Kibamba alikiri kuwepo kwa mvutano wa hapa na pale, baina ya Jukwaa na Tume, na kufafanua kwamba hauna athari kubwa kama inavyodhaniwa, kwani wanakubaliana katika mambo mengi.
Alisema tofauti ipo katika suala zima la mgongano wa kisheria, hasa kutofanyiwa marekebisho katika baadhi ya vipengele kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kama ilivyoahidiwa.
Alishauri kubezana kusipewe nafasi, kwa kuwa kunaharibu dhana ya kusikilizana, badala yake Tume ifanyie kazi maoni yao na kuyaheshimu hata kama wanaona hayana nafasi.
Alishauri pia Kanisa na taasisi nyingine za dini, kuunda mabaraza mara rasimu itakapotoka, ili kuruhusu watu kuichambua rasimu na kupeleka maoni kwa Tume, kabla ya hatua ya kuunda Bunge Maalumu la Katiba haijafanyika.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, wakati wowote kuanzia sasa, kulingana na muda uliowekwa kisheria, rasimu hiyo ya awali, itatolewa.

No comments:
Post a Comment