Tuesday, May 14, 2013

IKULU YATAKA WANANCHI KUPUUZA KAULI ZA SLAA...

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu.
Wananchi wameaswa kupuuza kauli ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akimtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuwa alisambaza sumu wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010.

“Kauli ya Slaa itabaki ni kauli tu inayostahili kupuuzwa na wananchi, itabaki ni kauli ya mtu mzima anayetapatapa na kufanya jitihada kubwa kujivunjia mwenyewe heshima kwa kutunga na kusambaza uongo,” ilisema taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es Salaam jana.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilimshauri Dk Slaa kama hana jambo la maana la kuwaambia wananchi ama ameishiwa hoja, ni vema akanyamaza, awaachie wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo, kuliko kuendeleza riwaya zake zisizokuwa na mashiko. “Yake ni santuri iliyochosha wananchi,” ilisema taarifa.
Jana, Dk Slaa alikaririwa na gazeti la Tanzania Daima,  akidai kuwa Rais Kikwete na timu yake ya kampeni, “ilikuwa ikisaka kura kwenye nyumba za ibada na kumwaga sumu mbaya ya udini ambayo sasa inaitesa Serikali na Taifa” kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
“Katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Dk Slaa amlipua JK” kwenye gazeti linalounga mkono Chadema, la Tanzania Daima, Slaa anadai kuwa migogoro ya sasa ya kidini, ‘inajengwa au kutengenezwa na Serikali iliyojikita kusambaza sumu ya udini katika misikiti wakati wa kampeni za urais mwaka 2010’”, ilisema taarifa.
Iliongeza kuwa hakuna namna nyingine ama bora zaidi ya kuielezea kauli hii ya Slaa isipokuwa kauli hiyo ni uongo mtupu.
Ilisema kauli ya Slaa ni mwendelezo wa mtiririko usiokuwa na mwisho wa ghiliba ambazo hazitafanikiwa za kuhadaa wananchi kuhusu ukweli wa mambo ulivyo nchini.
“Rais Kikwete na timu yake ya kampeni kamwe hawakufanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, ama wa mwaka mwingine wowote, katika nyumba yoyote ya ibada iwe msikitini au kanisani au hekaluni, mahali popote katika nchi yetu,” ilisema.
Ilisisitiza kuwa Rais hajawahi hata kufikiria kuchanganya dini na siasa. Hana sababu ya kufanya hivyo, kwa kuwa anaelewa fika madhara ya udini kwa mustakabali wa nchi, kwa umoja wa Taifa na kwa mshikamano wa wananchi wake.
“Yeyote anayejaribu kumbebesha Rais Kikwete msalaba wa udini ana lake jambo na ni vema atwambie fika Rais alitumia Msikiti upi, ama Kanisa lipi, mahali gani na kwa nyakati gani kufanya kampeni,” ilisema taarifa ya Ikulu.
Katika kinachoonekana ni azma ya makusudi ya kumchafua Rais Kikwete, hivi karibuni katika mkutano wa Bunge linaloendelea Dodoma, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alitoa kauli inayofanana na hiyo.
Lema alisema Rais Kikwete ndiye kinara wa udini nchini, na hata alipotakiwa kufuta kauli hiyo alikataa na ndipo Kiti cha Spika kilipompa siku saba atoe uthibitisho.

No comments: