HAYA NDIO MAJINA YA WAKURUGENZI WAPYA WA MIJI NA MAJIJI...
Hawa Ghasia. |
Majiji manne nchini yamepata wakurugenzi wapya baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko ya uongozi kwenye halmashauri za Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na Mbeya.
Katika mabadiliko hayo, Rais ameteua na kupandisha vyeo wakurugenzi wa mamlaka mbili za serikali za mitaa kuwa wakurugenzi wa majiji.
Aidha, amebadilishia vituo vya kazi kwa wakurugenzi wa majiji wawili ili kuongeza ufanisi wa utendaji. Mabadiliko haya yalianza Aprili 12.
Taarifa ya uteuzi huo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.
Alisema kwa uteuzi huo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Sipora Liana sasa anakuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Hassan Hida, anakuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza.
Aidha, Mussa Zungiza aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam anakwenda Mbeya, huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanza, Wilson Kabwe akihamishiwa Dar es Salaam.
Kwa mabadiliko hayo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya uteuzi kwa nafasi za wakurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Tabora na ya Mji wa Njombe zilizobaki wazi na kuwabadilisha vituo vya kazi baadhi ya wakurugenzi.
Mabadiliko hayo yanagusa halmashauri tano. Katika taarifa yake, Waziri Ghasia alisema Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Alfred Luanda sasa anahamia Tabora, wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Meatu, Isaya Mngurumi anakwenda Njombe na Mkurugenzi wa Mpanda, Joseph Mchina anakwenda Singida.
Boniface Nyambere aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ujenzi Mwanza, anakwenda Kigoma. Pia Mwanasheria Suleiman Lukanga aliyekuwa Tamisemi anakwenda Mpanda.
Waziri Ghasia, alisema katika kipindi cha kuanzia Desemba mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu, Waziri Mkuu ameteua wakurugenzi 18.
Alitaja majina yao na maeneo ya kazi kwenye mabano kuwa ni Hamisi Yunah (Busega), Twalib Mbasha (Monduli ), Mussa Natty (Kinondoni), Omari Mkombole (Babati), Danstan Mallya (Sengerema), Abdallah Kidwanka (Geita), Godwin Benne (Mlele), William Waziri (Ludewa) na Gaudence Nyamwihura (Liwale).
Wengine ni Grace Mbaruku (Lindi), Zabibu Shaban (Pangani), Amina Kiwanuka (Mkinga), Abdulrahman Mndeme (Nzega), Sixtus Kaijage (Songea), Rashid Salim (Rufiji) na makaimu ni Mwendahasara Maganga ( Ilala), Paul Ntinika (Mufindi) na Abdallah Malela (Bariadi).
Comments