![]() |
| Mtuhumiwa huyo akitolewa gerezani ndani ya gari maalumu chini ya ulinzi mkali. |
Mmoja wa wanaume wanaoshitakiwa kwa shambulio baya zaidi la ubakaji wa kundi dhidi ya mwanafunzi ndani ya basi amepigwa vibaya na kulishwa sumu na wafungwa wenzake na yuko mahututi hospitalini, mwanasheria wake ameeleza.
Mamlaka za gereza zilikanusha kutenda visivyo dhidi ya Vinya Sharma, ambaye amekuwa akishikiliwa kwenye gereza la Tihar mjini New Delhi tangu alipokamatwa kwa tuhuma za kumshambulia mwanamke huyo Desemba, mwaka jana, tukio lililoifadhaisha India na kusababisha maelfu ya watu kuandamana kwenye mitaa.
Mtuhumiwa mwenzake wa Sharma, Ram Singh, anayedaiwa kuwa kiongozi wa genge hilo, alikutwa amenyongwa ndani ya selo yake mnamo Machi, mwaka huu.
Polisi walielezea kifo chake kama cha kujitoa mhanga ingawa hukumu yake bado haijatolewa.
Mwanasheria wa Sharma, A.P. Singh, aliwashutumu wafungwa kwa 'kumpiga kifuani' na kumwekea sumu katika chakula chake, na alisema amelazwa kwenye Hospitali ya Lok Nayak Jai Prakash Jumanne baada ya kuwa ametibiwa katika hospitali nyingine jijini humo tangu Jumapili.
"Vinay alipigwa na wafungwa wenzake wanne au watano ndani ya majengo ya jela hiyo," alieleza, akiongeza kuwa alikuwa katika hali mbaya akiwa hajitambui.
Sunil Gupta, msemaji wa jela ya Tihar, alisema Sharma alikuwa akitibiwa kwenye hospitali moja ya jijini humo kutokana na maradhi ya homa.
"Hakukuwa na kipigo kama hicho dhidi ya Vinay kwa uelewa wangu. Madai yote hayo si ya kweli," alisema.
Polisi walimkamata Sharma na Singh, sambamba na wanaume watatu watu wazima na mvulana mmoja, kwa mashitaka ya kumbaka mwanafunzi wa udaktari ndani ya basi lililokuwa safarini na kumpiga vibaya yeye na rafiki yake wa kiume mnamo Desemba 16, mwaka jana.
Mwanamke huyo alifariki kutokana na majeraha yake hospitalini nchini Singapore wiki mbili baada ya shambulio hilo, ambalo limewachukiza wananchi wengi nchini India, ambao waliandamana kwa maelfu kwa siku kadhaa kudai sheria kali kupambana na uhalifu wa kijinsia.
Mahakama ya jipi hilo ambako Sharma alifikishwa kujibu mashitaka tangu mapema mwaka huu ilizitaka mamlaka za jela na madaktari Jumatano kuwasilisha ripoti kuhusu afya yake jana.
Sharma alihusishwa kimakosa katika kesi hiyo, mwanasheria wake alisema wakati wa kuanza kwa kesi hiyo.

No comments:
Post a Comment