BANDARI MPYA YA BAGAMOYO SASA YAKALIWA KOONI...

Ufukwe wa Bagamoyo ambako kunatarajiwa kujengwa bandari kubwa.
Siku chache tangu Rais wa China, Xi Jinping akubali kujenga bandari kubwa kusini mwa Afrika katika eneo la Bagamoyo, Mwakilishi wa Chake Chake, Omar Ali Shehe (CUF), ameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuzuia ujenzi huo.

Shehe aliyekuwa akiulizwa swali katika Baraza la Wawakilishi jana, aliitaka SMZ kuzuia ujenzi huo kwa maelezo kuwa ikijengwa, itaharibu mipango ya Zanzibar ya ujenzi wa bandari mpya ya Mpiga Duri mjini hapa.
Kwa mujibu wa Shehe, Zanzibar ilikuwa na wazo la kujenga bandari hiyo siku nyingi, lakini sasa Tanzania Bara, ‘imeipiku’. Alihoji kwa nini SMZ haikujenga hoja hiyo wakati Xi alipofanya ziara nchini.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi, alisema SMZ haina uwezo wa kuzuia ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, kwa sababu kila upande una mikakati yake ya kuimarisha sekta za mawasiliano na uchukuzi wa bandari.
Ussi alisema maandalizi ya ujenzi wa bandari hiyo, yako hatua za mwisho kwa msaada wa Serikali ya China. 
Alisema kwa sasa kazi kubwa inayofanywa na SMZ, ni kutafuta washirika wa maendeleo, watakaosaidia kuunga mkono ujenzi huo.
“Tayari ‘tumeuza’ mpango wetu wa ujenzi wa bandari kwa washirika wa maendeleo, ikiwamo michoro na sasa tunasubiri wao,” alisema.
Ussi alikiri kuwa bandari ya Malindi imezidiwa na mizigo, zikiwamo kontena  hivyo nia ya kujenga bandari mpya iko palepale.
Katika ziara ya siku mbili ya Rais Xi, Tanzania na China zilisaini mikataba 17, yenye manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.
Miongoni mwa mikataba hiyo, ni ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, inatarajiwa kuwa kubwa kuliko zote katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, na ujenzi wake utatumia dola za Marekani bilioni 10. 
Mikataba iliyosainiwa kunufaisha Zanzibar moja kwa moja ni katika ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi.
Makubaliano mengine ni pamoja na kuboresha hospitali ya Abdullah Mzee ya Zanzibar na makubaliano ya kuipa Zanzibar vifaa vya kukagua kontena bandarini.

No comments: