Friday, March 1, 2013

HATMA YA SHEKHE PONDA KUJULIKANA MACHI 5...

Shekhe Ponda Issa Ponda akisindikizwa na askari kuingia mahakamani.
Hatma ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Shehe Issa Ponda na wenzake 49, itajulikana Machi 5, mwaka huu wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itakapotoa uamuzi kama wana kesi ya kujibu au la.
Endapo washitakiwa watakutwa na kesi ya kujibu watatakiwa kupanda kizimbani kuanza kujitetea na kama hawana kesi ya kujibu wataachiwa huru.
Shehe Ponda na wenzake 49 wanakabiliwa na mashitaka matano, likiwemo la kupanga njama ya kutenda kosa, wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59, uchochezi, kuingia kwa jinai na kujimilikisha kiwanja cha Chang’ombe Markazi,  kinachomilikiwa na Kampuni ya AgriTanza.
Awali, Wakili wa Utetezi, Juma Nassoro akitoa hoja za majumuisho mbele ya Hakimu Victoria Nongwa, aliiomba Mahakama iwaone washitakiwa hawana kesi ya kujibu, kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kujenga kesi na kuthibitisha tuhuma dhidi ya washitakiwa.
Alidai kuwa polisi walifungua kesi hiyo ya jinai kwa jazba, kwa kuwa walikuwa na uwezo wa kuwashauri washitakiwa wakafungue kesi ya mgogoro wa ardhi katika Mahakama zinazotatua migogoro hiyo.
Wakili Nassoro alidai katika mashitaka ya kupanga njama na uchochezi, hati ya mashitaka haijaeleza washitakiwa walipanga na kushawishi kutenda kosa gani.  Aidha, alidai kuwa hakuna shahidi aliyeeleza ni jinsi gani washitakiwa walipanga njama na kuiba mali hizo.
Katika mashitaka ya kuingia kwa nguvu na kujimilikisha kiwanja hicho, alidai kosa hilo lingethibitishwa endapo kungekuwa hakuna mgogoro wa ardhi, lakini katika ushahidi wao wanaeleza kuwa washitakiwa walikwenda kwa ajili ya kukomboa eneo lao, jambo linaloonesha kulikuwa na mgogoro.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai wameleta ushahidi uliothibitisha, kuwa washitakiwa walipanga njama za kuingia na kujimilikisha eneo hilo, kwa kuwa walikaa hapo kwa siku saba na kujenga Msikiti, pia wamekiri kukamatwa katika eneo la tukio.
Alidai kwamba mshitakiwa Swalehe Mukadam alikiri katika maelezo ya onyo, kuwa aliwashawishi watu kwenda kuokoa kiwanja hicho.
Wakili Nassoro aliiomba Mahakama iwaone washitakiwa wana kesi ya kujibu na kuwaamuru wapande kizimbani kujitetea kwa tuhuma zinazowakabili.

No comments: