![]() |
| KUSHOTO: Hospitali anayodaiwa Nyaga kujitupa ghorofani. KULIA: Nyaga Mawalla. |
Siku mbili baada ya kifo cha mfanyabishara maarufu wa
madini wa jijini Arusha, Henry Nyiti, mfanyabiashara mwingine bilionea wa Jiji
hilo, Nyaga Mawalla ameripotiwa kujiua usiku wa kuamkia jana.
Kifo cha Nyiti kilichotokea usiku wa kuamkia Alhamisi,
kimeelezwa kimetokana na ugonjwa wa malaria uliompata akiwa katika migodi yake
katika kijiji cha Ipanko, wilayani Ulanga, Morogoro.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu zilisema Mawalla
mmoja wa mabilionea wenye umri mdogo akiwa hajafikisha miaka 40, alijirusha
kutoka ghorofa la Hospitali ya Nairobi, Kenya alikokuwa amelazwa kwa takribani
wiki mbili.
Tukio hilo, habari zilisema, lilitokea wakati akiwa
tayari ameruhusiwa kutoka hospitalini na alishamwita dereva wake tayari kwa
safari ya kurudi nchini.
Juhudi za mwandishi kupata taarifa za kina kutoka kwa
ndugu au washirika wake kikazi katika kampuni aliyokuwa akimiliki ya Mawalla
Group hazikuzaa matunda, kwani simu zao ziliita bila kupokewa.
Hata hivyo, mmoja wa watu wa karibu na marehemu ambaye
hakuwa tayari kutajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji wa familia,
alithibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa, ingekuwa vigumu kupata wasemaji kwa
kuwa karibu wote wako Nairobi kutokana na kifo hicho.
“Ni kweli hilo limetokea, lakini linatuchanganya, kwa
sababu amechukua uamuzi wa kujiua wakati alisharuhusiwa kutoka
hospitalini…sijui ni nini hasa kimemkumba,” alisema mmoja wa watoa habari wetu.
Alidokeza kuwa
mwili wa marehemu ulitarajiwa kuwasili jana jioni kwenye uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tayari kwa taratibu za mazishi nyumbani kwao
Marangu, Kilimanjaro.
Licha ya kuwa wakili na mfanyabiashara maarufu, alikuwa
pia mwalimu wa sheria, akifundisha kwa muda wa ziada katika Chuo Kikuu cha
Makumira.
Taarifa za misiba ya wafanyabiashara hao maarufu
zimeshitua wengi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambako walijijengea
mitandao mikubwa ya kibiashara.
Katika mitaa ya Arusha, taarifa za wafanyabiashara hao
zilionekana kugusa makundi mengi, kutokana na mikusanyiko isiyo rasmi iliyokuwa
inajadili vifo hivyo.
Mjadala uliibuka pia kwenye mitandao ya kijamii, wengi
wakichangia juu ya kifo cha bilionea huyo kijana.
Mmoja wa wachangiaji hao kupitia mtandao wa
jamiiforums.com, ameandika; "Marehemu Nyaga Mawalla alikuwa ana matatizo
ya pumu siku nyingi, na alikuwa anakwenda Nairobi kwa matibabu, inashangaza
kiasi fulani...maana alikwenda kikazi mpaka mauti yalipomkuta ambapo
inasemekana kajiua… hii ni kwa mujibu wa Mwanandugu wa marehemu.”
Mwingine ameandika; “Nimeweza kuongea na ndugu wa karibu
na ame confirm kwamba jamaa alifariki jana Nairobi Hospital ambapo alikuwa
amelazwa kwa takribani wiki mbili.
“Alikuwa amekwenda Nairobi kwa sababu dawa zake alizokuwa
anatumia zilikuwa hazifanyi kazi, kwa hiyo madaktari wakawa wamebadilisha dawa.
Akiwa Nairobi alikuwa amekataa kuonana na watu. Alikuwa anaonana na mdogo wake,
Casmir na dereva wake ambaye walikwenda wote.
“Jana (juzi) alikuwa na dereva wake siku nzima, ilipofika
mchana akamwambia aondoke chumbani ili apumzike. Huku nyuma aliruka kutoka
ghorofani kwa nia ya kujiua. Hatuwezi kujua pengine hizo dawa zilimfanya
achanganyikiwe akili au kuna lingine kubwa.”
Wakati haijafahamika siku ambayo Mawalla atazikwa, habari
kutoka kwa familia ya Nyiti aliyekuwa pia kada wa CCM, zilieleza kuwa mwili wa
mpendwa wao unatarajiwa kuzikwa kesho Tengeru, Arumeru, Arusha.

No comments:
Post a Comment