WAISLAMU WAASWA KUACHA MAANDAMANO...

Moja ya maandamano ya Waislamu jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Waislamu jijini Dar es Salaam, wameombwa kuepuka kushiriki maandamano yaliyoitishwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, yanayotarajiwa kufanyika kesho.
Mwito huo umetolewa jana na Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA) na Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation (TIPF).
Akisoma tamko la taasisi hizo jana, Mwenyekiti wa TIPF, Shehe Sadik Godigodi, alisema maandamano hayo yaliyolenga kushinikiza Katibu wa Jumuiya hiyo, Shekhe Ponda Issa Ponda, apewe dhamana, yatazidisha ugumu wa dhamana hiyo.
Badala yake, Shehe Godigodi aliahidi Bahakita na TIPF, zitasimamia mchakato wa kuhakikisha Shekhe Ponda anapata dhamana, kwa kuonana na DPP, Eliezer Feleshi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi.
Alifafanua kwamba, katika mazungumzo yao na Waziri na DPP, watashirikisha wanasheria wa Kiislamu, kwa kuangalia vigezo vitakavyotolewa na wao watakavyotetea.
Aidha, Shekhe Godigodi alisema watakutana na viongozi wa dini akiwemo Mufti, Shekhe Issa Simba,  Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Alex Malasusa.
Mkutano huo utahusu kutafuta muafaka wa migogoro ya kidini.
“Maandamano ni haki ya mtu kikatiba, lakini kwa uchunguzi tuliofanya taasisi yetu haya ya keshokutwa (kesho), yana lengo la vurugu hivyo hatuyaungi mkono  kwani yanaongeza ugumu hata katika kuomba dhamana ya Shehe Ponda,” alisisitiza.
Alisema suala la kesi ya Ponda lipo kisheria na lazima lishughulikiwe kisheria, kwani ni dogo na linaweka kupatiwa ufumbuzi, lakini siyo kuandamana na kusababisha vurugu na majeraha kwa Waislamu.
Mwenyekiti wa Bahakita, Said Mwaipopo, alisema   maandamano hayo yana mkono wa kisiasa, kwani jumuiya hiyo ilipofanya mkutano kujadili suala ya dhamana ya Ponda, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliwapatia Sh 300,000 na baadae wakaenda makao makuu ya Chadema, akawapatia Sh milioni 5.
Mwaipopo alisema mwingine ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye aliahidi kushughulikia dhamana ya Ponda, jambo lililofanya taasisi nyingine kusubiri matokeo ambayo mpaka leo hajasema lolote. 
“Hivi ni lazima tujiulize mkutano wa Waislamu kujadili kiongozi wao, walimualika  Mnyika wa nini?  Kwa nini aliwapatia fedha zote  hizo?” Alihoji Mwaipopo.
Mwandishi alipomtafuta Mnyika, ili azungumzie suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema yuko mbali na mbunge huyo na hawawezi kuzungumza jana. Simu ya Profesa Lipumba iliita bila majibu.

No comments: