Wednesday, February 6, 2013

WABUNGE WATAMANI WAACHIWE WADUNDANE BUNGENI DODOMA...


Kikao cha Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania kikiendelea mjini Dodoma.

Hadhi ya Bunge ambalo ni moja ya mihimili muhimu ya Dola, sasa imeanza kutiliwa shaka na wasomi na wananchi wa kawaida, kutokana na mwenendo wa wabunge uliokosa staha na ustaarabu wa uendeshaji wa vikao.
Wananchi wasomi na wa kawaida, walionesha hofu hiyo jana walipozungumza na mwandishi kuhusu mwenendo wa Bunge juzi na jana, uliooneshwa kwa wananchi moja kwa moja kupitia televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Baadhi ya wasomi walionesha hofu kuwa muhimili huo unaweza kugeuka wa kihuni, huku watu wa kawaida wakilifananisha na kipindi cha futuhi cha ze komedi.
Wakizungumzia hali ya Mkutano wa 10 wa Bunge hasa vikao vya juzi na jana, wasomi walieleza kuwa  ni matokeo ya siasa za kibabe, jazba na inatishia usalama wa muhimili huo.
Mkuu wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Adolf Mkenda, akizungumzia hali hiyo alisema: “Hakuna kitu muhimu kama kufuata kanuni, Spika na wabunge wa pande zote wanapaswa kutii kanuni, ubabe haujengi na kupiga kelele si suluhisho.”
Akifafanua kuhusu kauli yake, Dk Mkenda alisema Bunge halipaswi kuwa la kishabiki, kwamba Mbunge akifanya kitu cha ovyo, kwa kuwa ni wa upande fulani basi bila kujali maslahi ya wananchi, anaungwa mkono.
Aliongeza kuwa matokeo ya ushabiki wa aina hiyo, yatalipeleka Bunge kugeuka la kihuni. “Wabunge hawapaswi kufanya mambo kwa ushabiki, hoja za msingi ni vizuri zikafanyiwa kazi na wananchi wanataka kuona matokeo yake, si ushabiki.
“Wataishia kupigana kama mabunge ya wenzetu tunayoyashuhudia, hili suala la kanuni halimhusu mtu mmoja bali ni wabunge wote,” alisisitiza Dk Mkenda.
Alisema kanuni zingezingatiwa, hali ya kelele bungeni juzi isingepata nafasi na kuongeza kuwa wapinzani ambao waliongoza zaidi kupiga kelele, kutokana na kuondolewa kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Ubungo,  John Mnyika (Chadema), walipaswa kuwa waungwana.
Dk Mkenda alisema kelele zao zinawaweka katika hatari ya kuonekana wahuni, huku mhimili mzima ukiwa katika hatari hiyo pia.
Alisema hoja za msingi kama vile ya Mnyika ya tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam, hazipaswi kuchukuliwa kama kitu cha mzaha na kuishia kwenye vurugu bila mwafaka mzuri.
Profesa Mwesiga Baregu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (SAUT), alisema kilichotokea bungeni ni matokeo ya mambo yanayotokea katika jamii, yanayodhihirisha watu wamechoshwa na mambo yasiyotekelezwa.
“Kwa mwenye akili finyu, zile ni vurugu lakini ukiwa na mtazamo mpana yanafanana na yanayotokea katika jamii zetu leo, kama Mtwara, Iringa na kwingineko.
“Hali hiyo haijatokea tu Tanzania, historia ya mabunge ya dunia iko hivyo, cha muhimu ni kuondoa matabaka yanayosababisha wengine wadhani wanaonewa,” alisema Profesa Baregu.
Kama alivyoshauri Dk Mkenda, Profesa Baregu naye alishauri kanuni zifuatwe na kuzingatiwa kuliko kitu chochote.
Pia aliongeza kuwa, hoja za msingi zinazogusa maisha ya watu wanaowakilishwa katika mhimili huo na wabunge, zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.
Wananchi wa kawaida na baadhi ya wafanyabiashara wa kituo cha mabasi cha Mwenge, Dar es Salaam kwa nyakati tofauti walisema hawashangai kuona vurugu hizo zimehamia bungeni.
Wananchi hao walidai kuwa wanasiasa hao wamezoea kuwatumia katika kuongoza vurugu mitaani kwa kisingizio cha kudai haki ndio maana hawashangai kuona zimehamia bungeni.
“Kwa kweli mimi sishangai kuhusu yaliyotokea bungeni, unajua bwana, baadhi ya watu wanatumiwa na wanasiasa hao hao, sasa wananchi kwa muda mrefu tumekuwa tukiumia, acha na wao siku moja ‘wadundane’ (wapigane) ili wajengeane heshima,” alisema Nazir Mohamed, mfanyabiashara wa nguo Mwenge.
Huku akiungwa mkono na vijana wenzake waliokuwa wanamsikiliza, Mohamed alisema Bunge la Tanzania hivi sasa, linaelekea kupoteza mwelekeo na kuwa kama futuhi.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mohamed alisema aina hiyo ya Bunge ndiyo inayovutia wengi hasa vijana  kwa kuwa wamechoka na maisha.
Hata hivyo, mfanyabiashara mwenzake aliyejitaja kwa jina Jacob Mserera, alikuwa kinyume na wenzake na kueleza kusikitishwa na utovu wa nidhamu uliooneshwa na baadhi ya wabunge.
Mserera alishauri wabunge wakongwe waliomo bungeni, watoe mafunzo ya maadili kwa wabunge vijana, ili kuwarithisha mema.
Juzi, wabunge wengi wao wakiwa wa upinzani, walisimama bungeni wakati Naibu Spika Job Ndugai akiwa amesimama, kinyume cha kanuni za Bunge.
Kanuni hizo ziliweka bayana kwamba, Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti anapokuwa akiongoza kikao cha Bunge, akisimama mbunge yeyote aliyesimama anapaswa kukaa chini kusikiliza anachosema aliyekuwapo kwenye Kiti.
Kutokana na ukiukwaji huo wa kanuni, huku wabunge hao wakipiga kelele kama darasa la watoto watukutu, Ndugai  aliahirisha Bunge na kuagiza Kamati ya Bunge ya Uongozi ikutane kujadili hali hiyo.
Jana Spika, Anne Makinda alitoa maelezo kuhusu uamuzi wa Kamati, ikiwa ni pamoja na kulifikisha suala hilo katika Kamati ya Haki na Maadili na Madaraka ya Bunge, ili lifanyiwe kazi.
Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge, kurudia walichofanya juzi na kupiga kelele hali iliyosababisha Spika kuahirisha Bunge hadi leo.
Spika Makinda aliamua kuahirisha Bunge na kusitisha kujadili hoja binafsi katika mkutano huo kutokana na utovu wa nidhamu uliooneshwa juzi bungeni na kumlazimisha Ndugai, kuahirisha shughuli za Bunge kabla ya wakati.
Hoja binafsi iliyokumbwa na hatua hiyo, ni ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari (Chadema) ambayo ilitakiwa kuwasilishwa jana ikiitaka Serikali iunde kamati ndogo kuchunguza Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) namna linavyoathiri elimu nchini.
Akitangaza taarifa ya Kamati ya Uongozi bungeni jana, Spika Makinda alisema, uamuzi wa kutojadili hoja hizo ulifikiwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana kwa dharura juzi na kujadili vurugu zilizoibuka bungeni kwamba zilitokana na kujadili hoja binafsi.
“Kwa masikitiko makubwa sote tulishuhudia vurugu zilizojitokeza katika Bunge hili hasa wakati wa mjadala wa hoja binafsi za wabunge, kimsingi huu ulikuwa ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kutokea katika historia ya Bunge letu.
“Taasisi ya Bunge inalaani vitendo vilivyojitokeza jana vilivyovunja kanuni ya 60 (2) inayokataza Mbunge kuzungumza kabla ya kuruhusiwa na Spika na Kanuni ya 60 (12) inayowataka wabunge kukaa chini wakati wowote Spika anaposimama kutaka kuzungumza,” alisema.
Katika vurugu hizo za juzi, mvutano uliibuka wa kutumia kanuni kati ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Ndugai kuwa alimruhusu Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kutumia muda mwingi wakati ulitakiwa kutolewa kwa mtoa hoja, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema).
Katika vurugu hizo, wapinzani walikuwa wakidai Kiti cha Spika hakitendi haki kinaipendelea Serikali hivyo walisimama na kuimba CCM, CCM, kitendo ambacho kiliishia kwa kupiga kura na kuiondoa hoja ya Mnyika kwa kigezo kwamba haikuwa na uzito, kwani tayari Serikali ilishawekeza fedha nyingi katika miradi ya maji inayotekelezwa Dar es Salaam.
Spika Makinda alisema kutokana na vurugu hizo, Kamati ilifikia uamuzi wa kuzikemea kwa nguvu vurugu hizo ili kulinda heshima ya Bunge na kuhakikisha kwamba vitendo hivyo haviachwi vikaendelea na kusababisha madhara makubwa hata ya kupigana bungeni.
Kamati ilikubali pia suala la vurugu hizo lipelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ichunguze na kuleta mapendekezo bungeni kabla ya mkutano huu kumalizika.
Akitoa ufafanuzi alisema, tangu Januari 30 hadi Februari 4 Bunge liliamua kuruhusu kuwasilisha bungeni hoja binafsi za wabunge ambazo ziliahirishwa katika mkutano wa tisa kwa nia njema ya kujadiliana masuala makubwa ya kitaifa.
Alitaka wabunge wa kambi ya upinzani wasome kanuni za Bunge kwani, hoja binafsi za wabunge zinaongozwa na kanuni kuanzia ya 53 hadi 58 na ya majadiliano kuanzia 59 hadi 71 ambazo kwa ujumla wao zingefuatwa kama inavyotakiwa, vurugu zisingetokea bungeni.
Alisema, Kanuni za Bunge ya 54(1)-(2), zinaeleza wazi kuwa Mbunge anaweza kutoa hoja bungeni ili kupendekeza jambo lolote lijadililiwe na pendekezo hilo linatakiwa liwe limekamilika ili lipate uamuzi bayana wa Bunge.
Alisema  kifungu cha 53 (6) c kinaonesha wazi ikiwa hoja ni ya Serikali, msemaji wa kambi ya upinzani atapewa nafasi ya kutoa maoni juu ya hoja hiyo, na kama hoja si ya Serikali, basi Msemaji wa Serikali atapewa nafasi ya kutoa maoni ya shughuli za Serikali juu ya hoja hiyo kama Profesa Maghembe alivyopewa.
Kanuni ya 62  inabainisha kuwa muda utakaotumiwa na wazungumzaji mtoa hoja ana dakika 30 na anayetoa maoni ya  upande wa pili  anapewa muda wa dakika 30 kama ilivyofanyika kwa Profesa Maghembe kutoa maoni ya shughuli za Serikali.
Kuhusu madai kwamba Kiti kinatoa upendeleo wa wazi kwa Serikali dhidi ya upinzani, alisema jambo hilo si kweli, hata hivyo, alisisitiza kuwa kama uamuzi unaofanywa na Kiti una kasoro kanuni zinaruhusu mbunge ambaye hakuridhika na uamuzi huo, kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (4).
Mbunge Nassari alihoji kutojadiliwa hoja yake kwa kutumia kanuni namba 58 kwamba imeondolewa na Kamati ya Uongozi, lakini kikanuni inatakiwa iondolewe na mbunge husika, hoja ambayo Spika aliipangua kwa kusema Kamati ya Uongozi ina wajibu wa kupanga ratiba na ndivyo ilivyopanga.

No comments: