VIVUTIO VYA TANZANIA VYANG'ARA MAAJABU SABA AFRIKA...

Mlima Kilimanjaro.
Tanzania imeibuka kidedea katika shindano la Maajabu Saba ya Asili ya Afrika, kwa kuingiza maajabu matatu.
Mlima Kilimanjaro, Mbuga ya Wanyama ya Serengeti na Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, vilitamkwa jana kuwa miongoni mwa maajabu saba ya asili barani Afrika na kila moja ikiwa na sifa tofauti na nyingine.
Maajabu mengine ni Red Sea, Mto Nile ambao zawadi yake ilichukuliwa na Uganda kama asili ya mto huo na Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika sherehe hizo, Waziri Mkuu  Mizengo Pinda alisema Tanzania asilimia 20 ya ardhi yake, imehifadhiwa kwa ajili ya vivutio mbalimbali kutokana na heshima ya nchi katika kutunza vivutio vya asili.
Alisema hata ripoti ya Mkutano wa Uchumi Duniani (WEF) katika vivutio vya utalii, iliitaja Tanzania kuwa ya pili duniani kwa vivutio vizuri baada ya Brazili.
Sifa ya Kilimanjaro, ilitajwa kuwa Mlima mkubwa wa pekee duniani uliosimama peke yake na wenye theluji wakati uko katika ukanda wa Ikweta wenye joto. 
Serengeti ilitajwa kuwa na safari za wanyama aina ya nyumbu ya umbali mkubwa ambayo ni ya pekee ulimwenguni huku Ngorongoro ikitajwa kuwa hifadhi ya pekee duniani, yenye mazingira asilia ambayo wanyama pori na binadamu wanaishi pamoja bila kuathiriana.
Pinda alisema baada ya mashindano hayo, kazi ya Serikali ni kutunza vivutio hivyo na kuvitumia kupokea watalii wengi zaidi.
Ametaka Afrika kushirikiana na Tanzania kutangaza vivutio hivyo ili watu wanaotembelea Afrika, wapate fursa ya kushuhudia na kujionea vivutio hivyo.
Alimtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kumteua Dk Philip Imler, Rais na Muasisi wa Mashindano ya Maajabu Saba ya Dunia, kuwa Balozi wa Vivutio vya Tanzania Duniani.
Awali, Dk Imler alitaja wanyama saba wa ajabu Afrika, ambao wote wako Tanzania akiwemo Chui, Tembo, Mamba, Kifaru, Kiboko, Sokwe Mtu na Simba.

No comments: